31 July 2012
Siri hujuma mitambo ya TANESCO yafichuka
Na Benedict Kaguo, Dodoma
MBUNGE wa Mwibara Bw. Kangi Lugola (CCM), jana amefichua siri ya kuwepo mkakati unaoratibiwa na vigogo wa Shirika la Umeem Tanzania (TANESCO), ili kuharibu mitambo ya umeme kwa lengo la kumuumbua Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kutokana na msimamo alioweka kuhakikisha hakuna mgao wa umeme.
Bw. Lugola aliyasema hayo bungeni mjini Dodoma jana baada ya kuomba mwongozo wa Spika akitumia kanuni ya 68 (7) na kutaka kupata uhakika wa kauli ya Prof. Muhongo kuwa hakutakuwa na mgawo wa umeme ambao awali ulikuwa unatengenezwa mezani kwa faida ya kikundi cha watu wachache.
Alisema Prof. Muhongo amewaaminisha Watanzania kupitia Bunge lakini baada ya kauli hiyo, kumezuka kundi la watu wa TANESCO wakitaka kufanya hujuma ya mitambo ya umeme ili kuiwezesha nchi kuendelea kuwemo kwenye mgao.
Alisema hali hiyo inatokana na mafisadi kushindwa kulitumia Bunge kuhalalisha uozo wao hivyo zipo taarifa zinazodai hivi sasa wameamua kufanya hujuma kwenye mitambo hiyo.
Alisema suala la umeme ni nyeti na kuitaka Serikali kujipanga kukabiliana na hujuma hiyo kwani baadhi ya watu walitaka tatizo la umeme litangazwe kama janga la Taifa na nchi isiweze kutawalika.
Kwa upande wake, Mbunge wa kuteuliwa Bw. James Mbatia alisema hali ya sasa ni tete na kwamba suala la ufisadi ni mfumo ambao kuufumua kwa kauli peke yake ni vita kubwa kwani iko ndani ya Bunge na nje.
Alisema kutokana na vita hiyo ni vyema Serikali ikawapatia ulinzi wa uhakika Prof. Muhongo, Manaibu wake, Bw. Silvester Masele na Bw. Geogre Simbachawene, kwani wanaweza kuwawinda.
Bw. Mbatia alisema suala hilo ni nyeti hivyo ni vyema Serikali ikaliagiza Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kulinda mitambo na vyanzo vya umeme ili mafisadi wasiweze kutimiza lengo hilo.
Hata hivyo jana jioni, Naibu Spika wa Bunge Bw. Job Ndugai alimshukuru Bw. Lugola kwa kufichua mpango huo na kueleza kuwa suala la hujuma kwenye mitambo ni kubwa na kuiagiza Serikali ichukue hatua za haraka kuchunguza suala hilo.
Aliitaka Serikali ilifanyie kazi kwa haraka suala hilo ili kuzuia hujuma hiyo na kutaka ichukue hatua zikiwemo za vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha mitambo hiyo inakuwa salama.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Prof. Muhongo na wenzako hongereni kwa kaz nzuri ila nina wasiwasi na mfumo wa ubabe uliopo unaotumiwa na baadhi ya waheshimiwa kwenye kamati mbalimbali kwa manufaa yao na biashara zao binafsi sisi tunaomba kamati zote zivunjwe.
ReplyDeleteKazi nzuri sana Profesa Muhongo na wenzako mnafanya. Saidia Tz iondokane na balaa hili la giza katika karne hii. Mungu awatangulie katika kazi yenu.
ReplyDelete