26 July 2012
Mgombea ubunge apeleka malalamiko kwa Kikwete
Na Agnes Mwaijega
ALIYEKUWA mgombea wa ubunge katika Uhaguzi Mkuu 2010, Jimbo la Moshi Mjini, mkoani Kilimanjaro, kwa tiketi ya Chama cha NCCR-Mageuzi, Bw. Faustime Sungura, amewaandikia barua ya malalamiko viongozi wa Serikali akiwemo Rais Jakaya Kikwete.
Hatua hiyo imetokana na madai yake kwa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi iliyokuwa ikisikiliza shauri lake la kupinga matokeo ya uchaguzi yaliyompa ushindi mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Bw. Phileman Ndesamburo kuwa imekiuka sheria.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Bw. Sungura alisema kulikuwa na upendeleo wa wazi na ukiukaji wa sheria katika usikilizwaji wa kesi hiyo.
Alisema mwenendo wa kesi hiyo ambayo kwa sasa haipo mahakamani, unaonesha hata kama akiendelea kudai haki katika mahakama hiyo hawezi kuipata.
“Nimeamua kulalamika kwa kutumia njia za kiutawala kwenye ngazi zingine kutokana na hali ya upendeleo na ukiukaji wa wazi kabisa wa sheria ambao umefanywa na mahakama,” alisema.
Aliongeza kuwa, mahakama hiyo imekuwa ikimlinda Bw. Ndesamburo ili amalize muda wake wa miaka mitano hivyo kuacha kufuata misingi ya usikilizaji kesi za aina hiyo.
Bw. Sungura alidai kuwa, maamuzi ambayo yamekuwa yakitolewa na mahakama hiyo hayazinagatii sheria zilizopo na hayawezi kukatiwa rufaa bali yanapaswa kuombewa marejeo katika Mahakama Kuu iliyotoa maamuzi.
Alisema mbali na kumwandikia Rais Kikwete barua, pia ameandika kwenda Umoja wa Maifa (UN), Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Usalama wa Taifa, Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Jukwaa la Wahariri.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment