29 June 2012
Yanga yatema wachezaji 11 *Kujipima na Express ya Uganda kesho
Na Elizabeth Mayemba
KATIKA kuimarisha kikosi chake, uongozi wa Klabu ya Yanga umetema wachezaji 11 huku wengine wakipelekwa kwa mkopo katika timu nyingine.
Akizungumza Dar es Salaam jana Msemaji wa klabu hiyo, Louis Sendeu alisema leo wanatarajia kuwasilisha Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), majina ya wachezaji ambao wameachwa na wale watakaotolewa kwa mkopo katika timu nyingine.
"Mwishoni mwa mwezi huu, ndiyo mwisho wa kupeleka majina TFF ya wachezaji watakaoachwa hivyo kesho (leo), tutapeleka majina hayo katika shirkisho hilo," alisema Sendeu.
Aliwataja wachezaji ambao wameachwa kuwa ni Davies Mwape, Kenneth Asamoah, Julius Mrope, Idd Mbaga, Kigi Makassy, Atif Amour, Godfrey Bonny, Zuberi Ubwa, Abuu Ubwa, Bakari Mbegu huku Shaaban Kado akipelekwa kwa mkopo Mtibwa Sugar.
Sendeu alisema majina ya wachezaji wengine ambao watatolewa kwa mkopo, yatajulikana leo baada ya mchakato kukamilika.
Katika hatua nyingine, Yanga kesho inatarajia kucheza mechi ya kirafiki na timu ya Express ya Uganda kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika mchezo huo kiingilio kitakuwa sh.20,000 kwa VIP A, B na C sh. 15,000, Orange sh. 5,000 na bluu ni sh. 3,000.
Sendeu alisema mechi hiyo itakuwa ni kipimo kizuri kwa timu yake inayojiandaa na michuano ya Kombe la Kagame na Ligi Kuu Tanzania Bara.
Wakati huohuo, klabu hiyo leo itakuwa na kisomo kwa ajili ya kuwaombea marehemu wote ambao walikuwa wanachama, wakiwemo wachezaji, viongozi na wanachama.
Sendeu alisema kisomo hicho kitaanza saa saba mchana ambapo dua itasomwa na Katibu wa Baraza la Wazee wa Muafaka, Mzee Ibrahim Akilimali.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment