29 June 2012

Fiesta kufanyika katika mikoa 14



Na Victor Mkumbo

TAMASHA la burudani la fiesta, ambalo hufanyika kila mwaka kwa mwaka huu linatarajia kufanyika katika mikoa 14 ikiwa ni Tanzania Bara pamoja na Zanzibar.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana wakati wa uzinduzi wa tamasha hilo, Mkuu wa Vipindi wa Clouds, Sebastian Maganga alisema tamasha hilo linatarajia kuwa la aina yake kwa mwaka huu.


Alisema tamasha la mwaka huu limepewa jina la Serengeti Fiesta Super Nyota, ambalo lengo lake ni kuibua vipaji vya wasanii chipukizi.

Maganga alisema tamasha hilo linatarajiwa kuwa la aina yake kutokana na maandalizi yake ikiwa ni pamoja na ongezeko la mikoa.

Alisema Tamasha la Fiesta limeongezwa kwa mara ya kwanza mwaka huu katika mikoa ya Singida na Tabora ambapo halijawahi kufanyika.

"Kwa mwaka huu Tamasha la Fiesta, linatarajiwa kuwa la aina yake kutokana na maandalizi yake ambapo pia litakuwa tofauti kwani kuna zawadi za magari pamoja na pikipiki ambazo zitatolewa kwa mashabiki," alisema.

Naye Meneja wa Bia ya Serengeti ambao ndiyo wadhamini wakuu wa tamasha hilo, Allan Chonjo alisema kampuni yake inashirikiana na waandaaji wa Fiesta kwa miaka mitatu mfululizo.

Alisema Kampuni yake imetenga sh. milioni 150 kwa ajili ya zawadi kwa mashabiki watakaokuwa wakifuatilia Fiesta kwa karibu.

Chonji alisema tamasha hilo mwaka huu litavuka mipaka ambapo baada ya kumalizika nchini litarindima jijini Nairobi, Kenya kwa mara ya kwanza.

"Tumejipanga vizuri katika msimu huu kutokana na maandalizi ikiwa ni pamoja na maboresho zaidi," alisema.

No comments:

Post a Comment