20 June 2012
Waliompiga Manji kuwasilisha vielelezo leo
Na Zahoro Mlanzi
WAKATI mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa Klabu ya Yanga ukiendelea, wanachama walioweka pingamizi kwa baadhi ya wagombea wanaowania uongozi wa klabu hiyo akiwemo aliyekuwa Mfadhili wa klabu hiyo, Yusuph Manji wametakiwa kuwasilisha vielelezo vya pingamizi walizoweka kwa Kamati ya Uchaguzi ya klabu hiyo.
Shughuli hiyo ya kupokea vielelezo itaanza saa nne asubuhi makao makuu ya klabu hiyo mitaa ya Twiga na Jangwani na watatakiwa kutetea hoja zao.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa kamati hiyo Jaji Mstaafu, John Mkwawa alisema juzi saa 10 jioni ilikuwa ni siku ya mwisho ya kupokea pingamizi mbalimbali za wagombea uongozi wa klabu hiyo.
"Tunashukuru zoezi limekwenda vizuri na wapo wagombea waliowekewa pingamizi mgombea Yusuph Manji, ambaye anawania nafasi ya uenyekiti amewekewa pingamizi na wanachama watatu wenye kadi namba 007933, 008272 na 006225," alisema Mkwawa na kuongeza;
"Sara Ramadhani ambaye pia anawania uenyekiti naye amewekewa pingamizi na mwanachama mwenye kadi namba 003353 na 001702, lakini kwa pingamizi lililoletwa dhidi yake inaonesha walioweka wanataka ufafanuzi kama kiongozi aliyejiuzulu anaweza kugombea, hivyo hilo linahitaji ufafanuzi tu''.
Alisema mgombea Yono Kavela, ambaye anawania Makamu Mwenyekiti naye amewekewa pingamizi na mwanachama mwenye kadi namba 003974 na Ali Mayai ambaye anawania Ujumbe wa Kamati ya Utendaji.
Alisema baada ya kupokea pingamizi hizo, kamati imepanga siku ya leo kupokea ushahidi ambao unaweza kuwa wa binafsi au kwa maandishi (document) na si lazima aliyeweka pingamizi kuwepo siku hiyo.
Mkwawa alisema usaili utafanyika Juni 22, mwaka huu tofauti na ilivyopangwa awali kutokana na kutoa nafasi kwa kupitia vielelezo vya ushahidi vitakavyotolewa.
Alitoa hadhari kwa watu wanaoanza kufanya kampeni kabla ya siku hazijafika pamoja na wale wanaoingilia kamati hiyo katika shughuli zake.
Mbali na hilo, Mkwawa alizungumzia pingamizi la mwanachama Abeid Abeid 'Falcon', kwamba wamelitupia mbali kutokana na kujichanganya katika maelezo aliyoyawasilisha kwa kamati hiyo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment