25 June 2012

RC: Halmashauri hakikisheni hati chafu zinakoma




Na Allan Ntana, Tabora

MKUU wa Mkoa wa Tabora, Bi. Fatuma Mwassa, amezitaka halmashauri mkoani hapa kuhakikisha hazipati hati chafu kuanzia mwaka wa fedha ujao.

Alisema hati chafu zinachangia kuleta mashaka ya utendaji kazi wa watumishi katika halmashauri husika na kuharibu sifa zao.

Bi. Mwassa aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati akifungua kikao cha dharura cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga na kusisitiza kuwa, watendaji wazembe katika halmashauri zote mkoani hapa hawapaswi kuvumiliwa.

Aliipongeza Halmashauri ya Wilaya hiyo kwa ushirikiano mzuri wa watendaji wake ambao ndio umewezesha kupata hati safi mwaka 2010/11 na kukusanya mapato mengi katika vyanzo vya ndani.

Alisema hati chafu husababishwa na utendaji mbovu wa baadhi ya watumishi katika idara mbalimbali ambapo hali hiyo huchangiwa na uzembe wa Mkuu wa Idara husika hivyo kuruhusu uwepo wa dosari ndogo ndogo katika vitabu vya mahesabu.

“Ndugu zanguni, hizi dosari ndogo ndogo mnazozifumbia macho zinaathiri sana taarifa zenu za kifedha...zibeni mianya hii kuanzia sasa,” alisema Bi. Mwassa na kusisitiza kuwa, kuanzia mwaka ujao wa fedha hati chafu ni marufuku mkoani hapa.

Alitumia fursa hiyo kuzionya halmashauri zote kuacha tabia ya kukumbatia watendaji wazembe na wasio makini katika kutekeleza majukumu ya kazi zao.

“Waheshimiwa madiwani mnapaswa kuwa wakali pamoja na kukemea ipasavyo uzembe wowote unaofanywa na baadhi ya Wakuu wa Idara, naomba nipewe majina ya hao watendaji wazembe, nitawashughulikia mara moja.

“Kila mtendaji awe makini anapotekeleza wajibu wake, hatuwezi kufuga wezi, lazima tuoneshe mfano kwa kuwafukuza watendaji wazembe ili kurudisha nidha ya kazi kwa wangine,” alisema.

No comments:

Post a Comment