25 June 2012

Polisi atuhumiwa kuiba gari


Na Peter Ringi, Manyara

JESHI la Polisi mkoani Manyara, linawashikilia watu wawili akiwemo askari polisi Bw. Greison Gasper (26), mwenye namba PC G3629 wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), na mwenzake ambaye ni muosha magari Bw. Gabriel Alois (28), kwa tuhuma za kuiba gari aina ya Nissan Terano, yenye namba T993 ASX, mali ya Bw. Mstafa Athuman.


Kamanda wa Polisi mkoani Manyara, Kamishna Msaidizi Akili Mpwapwa, amethititisha kukamatwa kwa watu hao Juni 11 mwaka huu, Wilaya ya Ngara, mkoani Kagera, katika kizuizi cha Sekeseke wakilitorosha gari hilo kwenda wilayani Karagwe.

Alisema Juni 5 mwaka huu, mke wa Bw. Athuman alikwenda kuosha gari hilo eneo la Kanisa la Mungu na kuacha funguo kwa Bw. Alois lakini alipokwenda kulichukua, hakulikuta wala kumuona mtuhumiwa.

Kamanda Mpwapwa alisema mama huyo alitoa taarifa polisi ambao walianza kulitafuta na kufanikiwa kuwatia mbaroni watuhumiwa pamoja na kulikamata gari hilo.

“Watuhumiwa bado tunawashikilia na watafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika,” alisema Kamanda Mpwapwa.

No comments:

Post a Comment