27 June 2012

MOI waelemewa



Na Waandishi Wetu, Dar na mikoani

UONGOZI wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa (MOI), katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), umekiri mgomo wa madaktari kuathiriwa utoaji huduma za matibabu na kulazimika kutoa huduma za dharura pekee kwa kuwatumia madaktari bingwa.


Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Ofisa Uhusiano wa MOI, Bw. Almas Jumaa, alisema mgomo huo umesababisha huduma nyingine katika taasisi hiyo kusitishwa.

Alisema idadi ya madaktari wanaoingia kazini ni ndogo tofauti na siku za nyuma kabla ya mgomo.

“Mgomo huu umeathiri suala zima la utoaji huduma za matibabu, wagonjwa tunaowapokea ni wale dharura ambao wanatibiwa na madaktari bingwa,” alisema, Bw. Jumaa na kuongeza kuwa, huduma kwa wagonjwa wa kulipia hazitolewi kutokana na uhaba wa madaktari.

Aliongeza kuwa, madaktari viongozi ndio wanaofanyakazi ya kuzunguka wodini tofauti na awali ambapo kazi hiyo ilikuwa ikifanywa na madaktari wa ngazi zingine.

Katika Hospitali ya Mwananyamala, waandishi wetu walishuhudia mgomo baridi ukiendelea kutokana na wagonjwa kukosa matibabu kama walivyozungumza na Majira.

Kwa upande wa Hospitali ya Amana, hali ya mgomo ni kama juzi ambapo eneo ambalo madaktari huegesha magari yao, kulikuwa na magari machache ambapo katika Hospitali ya Temeke, hali ilikuwa tofauti na hospitali zingine kutokana na madaktari kuendelea na huduma kama kawaida.

Akizungumza na Majira katika Hospitali ya Muhimbili, aliyekuwa mbunge wa Arusha Mjini, Bw. Godbles Lema (CHADEMA),  alidai kukubaliana na uamuzi wa madaktari kugoma na wana madai ya msingi kwani mfumo wa nchi unawakandamiza baadhi ya watu.

Wakati huo huo, kutoka Geita, mkoani Mwanza, Chama cha Wafanyakazi wa Afya na Serikali Kuu (TUGHE), Tawi la Hospitali Wilaya kimewataka wafanyakazi kushiriki mgomo mgomo usiokuwa na kikomo hadi Serikali itakaposikiliza madai yao.

Chama hicho kilitangaza mgogoro huo juzi kwenye kikao cha wananchama kilichoshirikisha watumishi wa hospitali, vituo vya afya na zahanati.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kikao hicho, Mwenyekiti wa TUGHE, Bi. Mary Muntu, alidai uongozi dhaifu wa kupeana vyeo kirafiki, ndio umesababisha matatizo yao kuwa sugu.

Mwandishi wetu kutoka Mbeya anaripoti kuwa, madaktari mkoani humo wamekaidi agizo la Bodi ya Hospitali ya Rufaa la kuwataka wakutani ili wakae meza moja kujadili madai yao.

Mbali na mwito huo, hakuna daktari aliyejitokeza katika kikao hicho ambacho kilikuwa chini ya Mkuu wa Mkoa huo, Bw. Abbas Kandoro. Madaktari hao waliandikiwa barua ya mwito ili wafike katika kikao hicho kuzungumzia hatima ya madai yao lakini wamekataa.

Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi ya Hospitali hiyo, Kaimu Mkuu wa Mkoa huo, Dkt. Norman Sigalla, alisema bodi imefikia hatua hiyo baada ya kuona madaktari hao wamevunja mkataba ambao unawataka kufanya kazi bila kugoma.

Alisema mikataba hiyo itasitishwa kwa madaktari waliogoma hasa wale ambao wako kwenye mafunzo ya vitendo na kuwarejesha wizarani ambapo bodi imekaa na kugundua kuwa, mikataba hiyo imevunjwa hivyo kila mmoja ameandikiwa barua ya kujieleza.

Dkt. Sigalla aliongeza kuwa, kwa mujibu wa sheria za kazi, mtumishi asipofika kazini kwa muda wa siku tatu mfululizo anakuwa amejifuta kazi mwenyewe hivyo kama madaktari hao hawataripoti kazini watalazimika kuwaondoa.

Akizungumzia madaktari waliosajiliwa ambao wanashiriki mgomo huo, Dk. Sigalla, alisema wao watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria na Katibu Mkuu wa Wizara ambaye ndiye mwajiri wao.

Waandishi wetu wa mikoa ya Shinyanga na Kigoma wanaripoti kuwa katika mikoa hiyo, hakuna mgomo wa madaktari unaoendelea.

Habari hii imeandikwa na Esther Macha, Mbeya, Salma Mrisho, Geita, Rehema Maigala na Stella Aron, Dar es Salaa

No comments:

Post a Comment