25 June 2012

Mkurugenzi ashinda kesi ya kusimamia mali



Na Said Njuki Arusha

MAHAKAMA ya Mwanzo Maroboso mjini Arusha, imemthibitisha   Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Bw. Wilson Kabwe kuwa msimamizi halali wa mali ya marehemu ndugu yake aliyekuwa mfanyabiashara maarufu wa madini Bw. John Mkenga.

Bw. Mkenga alifariki Machi mwaka huu, kwa ajali ya gari ambapo licha ya familia kufanya kikao na kumteua Bw. Kabwe kuwa msimamizi wa marathi, mke wa marehemu Bi. Blandinja Mkenga aliibuka na kupinga uteuzi huo na kufungua kesi mahakamani.


Katika kesi hiyo, Bi. Mkenga alidai kutoshirikishwa katika kikao kilichompitisha Bw. Kabwe kuwa msimamizi wa mirathi hivyo Mahakama ililazimika kusikiliza shauri hilo namba 42/12.

Hukumu hiyo iliyotolewa mwishoni mwa wiki na Hakimu Bi. Mwanaidi Lemmy ambaye alisema, Mahakama haiwezi kuingilia maamuzi ya kikao halali cha ukoo.

Alisema Mahakama imezingatia baadhi ya malalamiko ya mke wa marehemu na kumteua kuwa Msimamizi Msaidizi wa mirathi hiyo.

“Kwa kuzingatia ushahidi uliotolewa na pande zote mbili, Mahakama imeridhika na kumthibitisha Bw. Kabwe kuwa Msimamizi Mkuu wa mirathi hii, mke wa marehemu atakuwa Msimamizi Msaidizi,” alisema Bi. Lemmy.


Aliongeza kuwa, mahakama hiyo imeona ni vyema Msimamizi Mkuu awe na upeo wa mambo ya sheria na mwaadilifu ili haki itendeke kwa pande zote ili mali zote zisimamiwe kwa umakini.

Bi. Lemmy pia aliagiza pande zote kuleta mashahidi wawili kila upande watakaothibitisha kuwa Msimamizi Mkuu ni ndugu halali wa marehemu na Bi. Mkenga ni mke halali wa marehemu waweze kutoa hati maalumu ya kuthibitisha uhalali wa wasimamizi hao.

Katika kesi hiyo ambayo iliibua hisia za watu wengi mjini hapa, Bw. Kabwe aliteuliwa kusimamia mirathi hiyo kwenye kikao cha ukoo kilichofanyika baada ya mazishi ya marehemu.

Baada ya siku kadhaa, Bi. Mkenga aliibuka na kupinga uteuzi wa awali wa kikao cha ukoo hivyo kufungua kesi mahakamani akipinga uteuzi huo kwa madai kuwa, uteuzi huo umelenga kuwapora mali za marehemu mume wake.

No comments:

Post a Comment