27 June 2012

Kesi ya Hassanoo yapigwa kalenda



Na Grace Ndossa

KESI inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA), Hassan Othman 'Hassanoo' na wenzake wawili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeahirishwa hadi Julai 27 mwaka huu.

Kesi hiyo iliahirishwa mahakamani hapo jana baada ya Hakimu aliyekuwa anasikiliza kesi  hiyo, Devotha Kisoka kujitoa kutokana na kuwa na majukumu mengine na kuikabidhi kwa Hakimu Theopili Mutakyawa.


Akisoma kesi hiyo mhakamani hapo jana Wakili  Mwandamizi wa Serikali, Elizabeth Kaganda mbele ya Hakimu Mutakyawa alisema kesi hiyo itasikilizwa kwa siku mbili mfululizo, ili aweze kutoa uamuzi kama kontena la shaba zinazodaiwa kuibiwa na watuhumiwa hao likabidhiwe kwa mwenye mali au la.

Hakimu Mutakyawa aliiahirisha kesi hiyo hadi  Julai 27 mwaka huu na Agosti 6 na 7, itaanza kusikilizwa mfululizo na kuutaka upande wa mashtaka kupeleka mashahidi.

Hasanoo, mfanyabiashara Wambura Kisiroti (32) na Dkt. Najim Msenga (50), ambaye ni mfanyabiashara wa madini na Salim Shekibula (29), ambaye ni mlinzi, wanakabiliwa na kesi ya wizi wa madini ya Shaba yenye thamani ya Sh400 milioni.

Awali Wakili Kaganda alidai mahakamani hapo kuwa Agosti 26, mwaka huu washtakiwa hao kwa pamoja walitenda kosa hilo eneo la Bahari Beach, wilayani Kinondoni.

Alidai washtakiwa hao waliiba tani 26 za madini ya shaba yenye thamani ya sh. milioni 400, mali ya Kampuni ya Liberty Express Tanzania Ltd yaliyokuwa yakisafirishwa kutoka Zambia kwa lori.


No comments:

Post a Comment