29 June 2012

HOSPITALI YA REGENCY

HOSPITALI ya Regency ya Dar es Salam imeanzisha program kabambe ya  upasuaji wa maradhi mbalimbali ya tumbo kwa njia ya teknolojia ya kisasa ya kutumia kamera, ambapo mgonjwa hapasuliwi sehemu kubwa.


Upasuaji huo unahusisha kupasua tundu dogo kwenye tumbo na kuingiza kifaa chembambe tumboni, ambacho huonesha picha ya tatizo husika kwenye televisheni na hatimaye daktari kufanya matibabu bila kupasua sehemu kubwa ya tumbo.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Hospitali ya Regency, Dkt. Rajni Kanabar, utaratibu huo mpya utapunguza gharama kwa wagonjwa kwenda India na nchi mbalimbali kwa ajili ya upasuji wa aina hiyo, ambao ndio kwanza umeanzishwa na hospitalini hapo.

“Badala ya kwenda nje ya nchi, kwa ajili ya upasuaji huu wa kisasa watu watapata fursa ya kufanyiwa upasuaji hapa hapa nchini, hii itaokoa fedha na muda na tangu tuanze huduma hii miezi miwili iliyopita wagonjwa 35 wameshapasuliwa na wanaendelea vizuri,” alisema Dkt. Kanabar.

Daktari bingwa anayefanya upasuaji huo, Dkt. Rajeev Tandon, alisema kwa upasuaji wa kawaida daktari hutegemea kufanya upasuaji mkubwa ili kufikia viungo anavyohitaji tumboni hali ambayo husababisha maumivu makali kwa mgonjwa na kutopona haraka.

“Upasuaji huu wa kisasa tunaofanywa hapa Regency, unamfanya daktari kufikia viungo anavyotaka kupitia matundu madogo tumboni, hii inasaidia mgonjwa kubaki bila makovu baada ya kupona, kupona haraka na kuendelea na shughuli zake saa moja tu baada ya upasuaji tofauti na upasuaji wa kizamani ambapo humchukua muda mrefu mgonjwa kupona,” alisema, Dk Tandon

Mmoja wa wagonjwa waliofanyiwa upasuaji wa aina hiyo Juni 21, mwaka huu, alisema alikuwa akisumbuliwa maumivu makali na kutapika kwa miezi kadhaa, lakini baada ya upasuaji anaendelea vizuri.


No comments:

Post a Comment