28 June 2012

CHANETA yazitaka timu kuwasilisha usajili


Na Amina Athumani

CHAMA cha Netiboli Tanzania (CHANETA), kimezitaka timu zote zitakazoshiriki michuano ya Ligi Daraja la Kwanza ziwe zimesilisha fomu za usajili wa wachezaji kuanzia Julai Mosi, mwaka huu.

Michuano hiyo imepangwa kufanyika Agosti, mwaka huu jijini Mbeya na itashirikisha timu 20 zilizopanda daraja kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania.


Akizungumza Dar es Salaam jana, Kaimu Katibu Mkuu wa chama hicho, Rose Mkisi alisema kuanzia Julai Mosi timu zote zifanye hivyo  kwa ajili ya kuhakikiwa ili kuepusha usumbufu katika michuano hiyo.

Alisema pamoja na fomu hizo timu zitatakiwa kuambatanisha sh. 60,000 kwa ajili ya vitambulisho vya wachezaji mara baada ya kuhakikiwa na kufanyiwa usajili.

Rose alisema maandalizi yote ya mashindano hayo yapo chini ya chama cha netiboli Mbeya, ambacho ndicho kilichopewa dhamana ya kuandaa michuano hiyo.

Alizitaja baadhi ya timu zilizopanda daraja na zitakazoshiriki michuano hiyo ni Tumaini, JKT Mbweni, Jeshi Stars, Hamambe Mbeya, Polisi Mbeya, Polisi Dodoma, Polisi Morogoro, Magereza Morogoro, Filbert Bayi, Ras Lindi, Ras Mtwara pamoja na timu nyingine.

No comments:

Post a Comment