29 June 2012
Bi. Kidude kupagawisha Temeke leo
Na Anneth Kagenda
NGULI wa muziki wa taarabu nchini, Kidude Binti Baraka 'Bi. Kidude', leo anatarajia kupagawisha wakazi wa Temeke katika shoo maalumu ya usiku wa taarabu.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Bi. Kidude alisema usiku huo utakuwa wa aina yake kwa kuwa amejipanga vya kutosha kuhakikisha anavurumisha burudani ya nguvu kwa mashabiki wa muziki wa taarabu.
Bi. Kidude ambaye aliwasili Dar es Salaam usiku wa kuamkia juzi akitokea Zanzibar kwa ajili ya shoo hiyo alisema wapenzi wa muziki wa mwambao wategemee mambo mazuri, kwani nyimbo zake amezitunga yeye mwenyewe na si kutoka kwenye vitabu.
"Nyimbo ninazotegemea kutumbuiza ni pamoja na ule wa Yalaiti, Alan miladura, Muhogo wa Jang'ombe na Halfa.
"Kutokana na umahiri nilionao ni kutokana na kutumia akili hivyo ninawaomba waimbaji taarabu kuiga mfano wangu wa kutumia akili na si vitabu," alisema.
Naye Mratibu wa shoo hiyo Thabit Abdully, alisema wamejiandaa vya kutosha kwani mbali na nguli huyo, pia kutakuwa na kundi la East African Melody wakiongozwa na Khadija Kopa, Maryam Hamisi Hammer Q, Mwanahawa Ally na wasanii wengine.
Alisema kiingilio kitakuwa sh. 5,000 na kama hali itakwenda vizuri shoo hiyo itakuwa ikifanyika kila Ijumaa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment