24 May 2012

Twiga Stars waelekea Ethiopia


Na Mwali Ibrahim

TIMU ya Taifa ya soka ya Wanawake 'Twiga Stars' inatarajia kuondoka nchini leo kuelekea Ethiopia kwa ajili ya kucheza mechi ya mchujo  wa fainali za Afrika kwa Wanawake (AWC) dhidi ya Ethiopia, mechi itachezwa  Mei 27 mwaka huu, kabla ya kurudiana wiki mbili baadaye jijini Dar es Salaam.

Timu hiyo itaondoka nchini ikiwa tayari imeshacheza michezo miwili ya kirafiki ya Kimataifa miwili na timu ya Afrika kusini 'Banyana Banyana' ambayo iliwafunga mabao 5-2 na timu ya Zimbabwe yenyewe iliwafunga mabao 4-1, michezo yote ilichezwa Uwanja wa Taifa,Dar es Salaam.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Kocha msaidizi wa timu hiyo Nasra Mohamed alisema, kutokana na matokeo hayo waliyoyapata waliyachukua kama changamoto kwao na tayari wameishafanyia marekebisho.

"Tumeshafanyia kazi upande wa ushambuliaji ambao ndiyo ulionekana umelega lakini pia ni pamoja na kufanya marekebisho katika kila eneo ili kuhakikisha tunapeleka kikosi kilicho kamilika," alisema.

Alisema, kwa niaba ya timu nzima watahakikisha wanapoondoka nchini leo wanakwenda kuiwakilisha vyema nchi katika mashindano hayo na kuipeperusha bendera ya nchi ipasavyo.

Aliongeza kuwa katika kambi waliyokaa Mlandizi tangu Aprili hadi sasa wamepata mazoezi ya kutosha na kikosi kipo katika hali nzuri ya kushiriki katika mashindano hayo.

Wakati huo huo timu hiyo imekabidhiwa mfano wa hundi wa sh. milioni 30 pamoja na vifaa vya michezo vyenye thamani ya sh. miliomi 5.5 na Benki ya NMB kwa kushirikiana na kampuni ya bia ya Serengeti (SBL) ambapo sambamba na hilo NMB imefungua akaunti ya changia Twiga stars kwa ajili ya kutoa fursa kwa wadau kuichangia timu hiyo.

Pia Serikali imewalipa wachezaji wa timu hiyo posho za siku 19 ili kuwajengea morali zaidi katika mchezo huo wa kimataifa.

No comments:

Post a Comment