08 May 2012

Simba, Yanga zaingiza mil. 260/-


Na Zahoro Mlanzi

MECHI ya Ligi Kuu Bara iliyowakutanisha watani wa jadi, timu za Simba na Yanga iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 260,910,000 huku kila timu ikipata sh. 62,646,395.

Mchezo huo ulikuwa ni moja kati ya michezo ya kufunga pazia la ligi hiyo uliochezwa juzi ambapo Simba iliweka historia nyingine kwa kuibuka na ushindi mnono wa mabao 5-0.


Kwa ushindi huo, Simba ambayo ilishatwaa ubingwa huku ikiwa na mechi moja mkononi, imefanya ubingwa huo kuwa na raha ya aina yake baada ya kuifunga Yanga.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari Dar es Salaam na Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura ilieleza kwamba mechi hiyo ilihudhuriwa na watazamaji 41,733.

"Viingilio katika mechi hiyo vilikuwa sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya bluu na kijani, sh. 10,000 viti vya rangi ya chungwa, sh. 20,000 VIP C, sh. 30,000 VIP B na sh. 40,000 VIP A ambapo watazamaji 36,980 walinunua tiketi za sh. 5,000 wakati 203 walikata za sh. 40,000," alisema Wambura.

Alisema kutokana na mapato hayo kila timu ilipata sh. 62,646,395, asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ni sh. 39,799,830 wakati TFF ilipata sh. 19,908,361.

Alisema gharama za mechi kabla ya mgawo ni nauli ya ndani ya waamuzi na kamishna sh. 20,000, posho ya kujikimu kwa kamishna sh. 40,000, mwamuzi wa akiba sh. 30,000, gharama za tiketi sh. 8,539,950.

Pia alisema maandalizi ya uwanja ni sh. 400,000, umeme sh. 300,000, ulinzi na usafi wa uwanja sh. 2,350,000 na Wachina ni sh. 2,000,000.

No comments:

Post a Comment