08 May 2012
Habert Marwa: Timu ya Yanga wapewe kuongoza vijana
Na Elizabeth Mayemba
KUFUATIA kipigo cha mabao 5-0 dhidi ya Simba, mmoja wa aliyekuwa Mjumbe wa Kamati ya Mashindano ya klabu ya Yanga Habert Marwa,baada ya kuonyesha kusikitishwa sana na kipigo hicho, alisema ili timu hiyo iwe na mafanikio makubwa haina budi iongozwe na vijana.
Akizungumza Dar es Salaam jana na mwandishi wa habari hizi baada ya kuhojiwa Marwa alisema, ili timu iwe na hadhi yake ni lazima iongozwe na isimamiwe na vijana ambao ndiyo nguvu kazi.
"Kama jina lenyewe la timu Young Africans, hivyo nguzo ya ushindi ni vijana kama ilivyo pia kwa wachezaji, kama uongozi utasajili wachezaji wazee lazima timu ifanye vibaya, lakini wakisajili wachezaji wenye umri mdogo watafanya vizuri katika mashindano mbalimbali ya kitaifa na kimataifa kwa kuwa watakuwa ni damu changa," alisema Marwa.
Alisema timu inapofungwa wanaoumia na kusononeka wengi wao ni vijana ambao pia hujitolea kwa hali na mali kuichangia timu kimapato kwa kulipia viingilio na kuishangilia timu yao inapocheza.
Kwa hali hiyo Marwa alishauri vijana wenye moyo na jitihada za namna hiyo ndiyo wanaostahili kupewa jukumu la kuiongoza Yanga.
Marwa alisema Mwenyekiti wa klabu hiyo, Llloyd Nchunga alifanya kosa kubwa sana kuwakabidhi wazee timu bila kushauriana na vijana baada ya uongozi wake kushindwa.
"Tunaamini kabisa wazee wanamawazo mazuri sana ya kuushauri uongozi unapokuwa na dhamira sahihi ya ushindani, kwani uzoefu walioupata enzi hizo wakiwa viongozi tena vijana ungewasaidia viongozi kwa wakati huu kufanya vizuri," alisema.
Alisema aliyewahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo Davis Mosha ambaye alijiuzulu wadhifa huo, alijitahidi kwa kiasi kikubwa kuwashawishi na kuwashirikisha yeye na vijana wengine kuchangia kwa fikra na uwezo wa kiuchumi pamoja na nguvu kazi ili timu hiyo iweze kupata mafanikio na hadhi yake pindi tu baada ya yeye kuchaguliwa.
"Baada ya Mosha kujiuzulu wengi wao na mimi nikiwemo tulijiuzulu siku moja baada ya yeye kujiuzulu," alisema
Pia aliwaasa vijana kujitokeza kwa wingi kwenda kuchukua kadi za uanachama wa klabu hiyo, badala ya kuwa mashabiki tu ili wapate fursa ya kuchagua viongozi bora na imara.
Hata hivyo alipoulizwa uwepo wake ndani ya klabu hiyo alisema "Baada ya kujiuzulu niliendelea kuwa mwanachama na shabiki kama ilivyokuwa awali, ikiwa na kutoa mawazo kama nilivyotoa mchango wangu huu wa mawazo kwa sasa,"alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEjkhriZg5qJXBiZD38yaukF105H1Q8MbZOV2K5tB9EUzLVryYlLxL_b3-EItuzfNPM-95aZVYHq8RyG8z5PCusQ5wKg1IOPpgBMzWkIzsPFdC1QhfmEW6wZe9nrMqGZZ-cSLu0aP_aOZTg/s760/times+fm.jpg)
No comments:
Post a Comment