02 March 2012

Siyoi ashinda tena Arumeru

*Abebwa juu juu, wanachama CCM washangilia ushindi huo
*TAKUKURU yanasa watatu katika uchaguzi, RC ahusishwa


Na Pamela Mollel, Arusha
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), Jimbo la Arumeru Mashariki, mkoani Arusha, kimemteua kwa mara nyingine Bw. Siyoi Sumari,
kuwania ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya chama hicho katika uchaguzi mdogo uliopangwa kufanyika Aprili mosi mwaka huu.

Uchaguzi huo umerudiwa jana baada ya ule wa awali ambao ulimpa ushindi Bw, Sumari, kupingwa na Kamati Kuu ya chama hicho CC kwa madai kuwa, kura za mshindi wa kwanza na pili, hazikuzidi asilimia 50.

Katika uchaguzi uliofanyika jana, Bw. Sumari ambaye ni  mtoto wa aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo marehemu Jeremiah Sumari alipata kura 761 wakati mpinzani wake Bw. William Sarakikya alipata kura 361. Uchaguzi huo ulianza saa nne asubuhina matokeo yalitangazwa saa 12 jioni.

Kura zilizopingwa katika uchguzi huo zilikuwa 1,124, kati ya hizo mbili ziliharibika. Matokeo hayo yalitangazwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Bw. Pius Msekwa.

Uchaguzi huo pia ulihudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, Kapteni mstaafu, Bw. John Chiligati. Baada ya kutangazwa matokeo hayo, wanachama wa CCM jimboni hapa walishangilia ushindi huo kwa kumbebea juu Bw. Sumari.

Akizungumza na waandishi wa habari, Bw. Sarakikya alimpongeza Bw. Sumari kwa ushindi aliopata na kusisitiza kuwa, anakubaliana na matokeo kama yalivyotangazwa.

TAKUKURU yanasa watatu

Wakati huo huo, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), mkoani Arusha, inawashikilia wana CCM watatu akiwemo aliyekuwa mgombea ubunge Jimbo la Arumeru Mashariki kwa tiketi ya chama hicho katika kura za maoni, Bw. Elirehema Kaaya, wakituhumiwa kugawa fedha.

Inadaiwa kuwa, Bw. Kaaya ambaye pia ni Katibu Mwenezi wa chama hicho Wilaya ya Nyamagana, mkoani Mwanza na wenzake, walikutwa wakigawa fedha ili kushawishi wajumbe wamchague mgombea wao katika marudio ya kura za maoni jimboni humo.

Kamanda wa TAKUKURU mkoani hapa, Bw. Mbengwa Kasomambutu, alisema mfanyabiashara maarufu wa madini ya Tanzanite na Diwani wa Kata ya Mbughuni, Bw. Thomas Mollel maarufu kwa jina la 'Askofu', naye amekamatwa.

“Watuhumiwa wote walikutwa kwenye kikao ambacho kinadaiwa kilikuwa na dhamira ya kugawa fedha kwa wajumbe walioshiriki uteuzi wa awali wa nafasi ya ubunge kwa tiketi ya CCM.

“Bw. Mollel alikabidhiwa fungu la fedha kwa ajili ya kushawishi  kundi la madiwani Jimbo la Arumeru Mashariki ili wampigie kura mmoja wa wagombea (jina tunalo),” alisema.

Alimtaja mwanachama mwingine wa CCM aliyekamatwa kuwa ni Bw. Joseph Mollel, ambaye ni Katibu wa Umoja wa Vijana UVCCM, Wilaya ya Monduli na mjumbe wa kikao hicho.

Alisema kikao hicho hakikumalizika vizuri kutokana na wajumbe waliopaswa kupewa fedha hizo, kugomea ushawishi huo wakidai kiasi walichotengewa hakitoshi.

“Askofu alifika kwenye kikao na kudai yeye ni mjumbe tu ila ameombwa awashawishi wajumbe hao wakubali kufanya ujanja wowote ili mgombea husika apite kwa madai kuwa kama hilo litafanikiwa mambo yao yatanyooka maana Mzee amesafiri kwenda Ujerumani,” alisema mmoja wa wajumbe walioshiriki kikao hicho.

Bw. Kasumambutu aliongeza kuwa, mtuhumiwa mwingine aliyekamatwa na kuhojiwa ni aliyekua mgombea wa nafasi hiyo ndani ya CCM kabla uchaguzi huo haujarudiwa Bw. Elishiria Kaaya.

Alisema baada ya kuhojiwa, alikutwa na tuhuma za kupewa jukumu la kuwashawishi wajumbe wote waliompigia kura katika uchaguzi wa awali kwa kuwapa rushwa ili wahamishie kura zao kwa mgombea mwingine (jina tunalo).

Aliongeza kuwa, TAKUKURU inaendelea kuwatafuta watuhumiwa watatu ambao walikimbia katika na kutelekeza pikipiki walizokuwa wakizitumia baada ya kukurupushwa na wenzao kukamatwa.

Kikao hicho alichokiita haramu, kilikuwa kikifanyika katika baa ya Levis iliyoko Kata ya Maji ya Chai na pikipiki hizo zinashikiliwa.

Katika kikao chake na waandishi wa habari, Bw. Mollel (Askofu) alimtupia lawama Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Bw. Magessa Mulongo kuwa ndiye aliyehusika kuwatuma TAKUKURU kwenda kuwakamata.

Akijibu tuhuma hizo, Bw. Mulongo alisema, taasisi hiyo inayojitegemea hivyo hana mamlaka ya kuwaagiza kufanya kazi na kuwataka wale wote waliokamatwa kwa tuhuma hizo wajibu tuhuma zao kwa mamlaka hiyo badala ya kuanza kutafuta mchawi.

Alisema taasisi hiyo iko kwa ajili ya kila mtu bila kujali kuwa yeye ni nani, hivyo mtu hapaswi kuanza kuzua madai yasiyo na msingi kwa kumtuhumu kuwa anahusika na kukamatwa kao.

“Askofu na wenzake wajibu tuhuma zao, kama umekamatwa ugoni na mke wa mtu, usiseme hapa lazima fulani anahusika kunitaja, bali jibu tuhuma za kukutwa ugoni na mke wa mtu usitafute mchawi sisi wote ni wateja wa TAKUKURU,” alisema, Bw. Mulongo.
    
   

1 comment:

  1. Takukuru, jihadharini na nyie msije mkapewa rushwa au shinikizo kutoka juu.

    Msicheleweshe uchunguzi maana na uchelewishaji nao ni RUSHWA kubwa zaidi.
    Hongereni kwa kujaribu maana inahitaji moyo.

    ReplyDelete