06 March 2012

Milovan: Pumzi tatizo Simba

Na Elizabeth Mayemba
KOCHA Mkuu wa Simba, Mserbia Milovan Cirkovic amekiri kuwa kikosi chake hakina pumzi na ndiyo maana mara nyingi wanafungwa mabao dakika za lala salama, hivyo anakazi ya ziada ya kuhakikisha tatizo hilo halijitokezi tena.

Juzi wakati timu yake ilipocheza na Kiyovu ya Rwanda katika mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho (CAF), Simba walionekana kulemewa dakika 15 za mwisho, hali ambayo iliwapa nafasi wapinzani wao kupata bao.

Katika michuano hiyo, Simba wamefanikiwa kusonga mbele baada ya kuwafunga Kiyovu kwa jumla ya mabao 3-2. Ugenini walitoa sare ya bao 1-1 na juzi walishinda mabao 2-1 jijini Dar es Salaam.

Akizungumza Dar es Salaam juzi, mara baada ya mchezo huo kumalizika, Milovan alisema wachezaji wake walikosa pumzi dakika za mwishoni, hivyo ana kazi ya ziada kabla ya mechi zao za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kuanza.

"Wachezaji wangu hawana pumzi za kutosha na ndiyo maana katika mchezo wetu na Kiyovu, dakika kama 15 za mwisho tulilemewa, lakini nitahakikisha tatizo hilo halijitokezi tena," alisema Milovan.

Alisema baada ya kumaliza raundi hiyo ya kwanza ya Kombe la Shirikisho, sasa akili zote anahamishia kwenye mechi za Ligi Kuu, lengo likiwa ni kufanya vizuri na kuendelea kubaki kileleni.

"Sasa tunatakiwa kuhamishia nguvu kwenye mechi zetu za Ligi Kuu, naimani kabisa wachezaji wangu watacheza kwa kujituma ili tuendelee kukaa kileleni mwa ligi hiyo," alisema.

Katika msimamo wa Ligi Kuu, Simba wanaongoza wakiwa na pointi 37 sawa na Yanga tofauti ikiwa kwenye mabao ya kufunga na kufungwa.

Baada ya kuvuka hatua hiyo kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho, Simba wataingia uwanjani tena kati ya Machi 23 au 25 mwaka huu kutavaana na ES Setif ya Algeria kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam


No comments:

Post a Comment