19 March 2012

Majambazi yavamia kijijini kwa Pinda

*Yajeruhi Ofisa Mtendaji, Mwenyekiti wa kijiji
Na Mwandishi Wetu, Rukwa
WATU wanne wanodaiwa kuwa majambazi, juzi usiku walifanya
walivamia nyumba ya Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Kibaoni Bw. Ladslaus Munguwajua (37), jirani na nyumbani kwa Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda, kilichopo Kata ya Usevya, tarafa ya Mpibwe, Wilaya ya Mpanda, mkoani Rukwa.

Akizungumzia tukio hilo, Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Jacob Mwaruanda, alisema watu hao walikuwa na bunduki ambayo haikujulikana mara moja pamoja na marungu.

“Watu hawa walimshambulia Bw. Munguwajua kwa kumpiga kichwani na marungu wakimlazimisha awape fedha lakini walifanikiwa kupora fedha taslimu sh. milioni moja.

“Huyu Mtendani ni mfanyabiashara, pia walimlazimisha awapatie funguo za kasiki la kuhifadhia fedha, baada ya kulikuta nyumbani kwake,” alisema Kamanda Mwaruanda.

Aliongeza kuwa, baada ya Bw. Munguwajua kubanwa atoe funguo na kudai zimepotea, watu hao walijaribu kulifungua lakini walishindwa na kuamua kuondoka.

Kamanda Mwaruanda alisema watu hao pia walimjeruhi mkononi Mwenyekiti wa kijiji hicho Bw. Gaston Kamina (52), ambae alikuwa nyumbani kwa Bw. Munguwajua akiangalia televisheni.

“Bw. Kamina alipata matibabu katika zahanati ya kijiji na kuruhusiwa ila Bw. Munguwajua alipelekwa Hospitali ya Wilaya ya Mpanda kwa matibabu na kuruhusiwa,” alisema.

Alisema baada ya polisi kupata taarifa, walifika eneo la tukio na kufanya msako ambapo watu wawili Bw. Wilembo Salum (35), na Bw. Kheri Obeid (30), walikamatwa wote wakulima wa kijiji jirani cha Usevya.

Aliongeza kuwa, katika eneo la tukio kuliokotwa maganda mawili ya risasi za SMG/SAR ambapo watu waliokamatwa bado wanahojiwa na uchunguzi unaendelea.

“Jeshi pa Polisi linaendelea kuwasaka watuhumiwa wengine walihusika na uvamizi huu,” alisema.

Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa huo, Mhandisi Stella Manyanya amemwagiza Kamanda Mwaruanda kuhakikisha watu waliofanya uvamizi huo wanasakwa.

“Lazima watuhumiwa wasakwe ili wafikishwe katika vyombo vya sheria, Mkoa huu si kimbilio la waharifu hivyo tutazidi kuimarisha ulinzi,” alisema Mhandisi Manyanya.


No comments:

Post a Comment