Na Zahoro Mlanzi
KOCHA Mkuu wa timu ya Kiyovu ya Rwanda, Baptist Kayiranga amevutiwa na kiwango kilichooneshwa na wachezaji wa Simba, Juma Kaseja, Mwinyi Kazimoto, Emmanuel Okwi na Ramadhan Singano na kudai anaweza kuwasajili ili kuimarisha kikosi chake.
Timu hizo zilikutana juzi katika mechi ya awali ya Kombe la Shirikisho na Simba kuibuka na ushindi wa mabao 2-1, hivyo kusonga mbele kwa jumla ya mabao 3-2 ambapo sasa itaumana na timu ya ES Setif ya Algeria.
Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mechi hiyo iliyopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Kayiranga alisema awali kabla hawajacheza na Simba alikabidhiwa majina matatu ambayo ni Kaseja, Okwi na Kazimoto na hata walipocheza mechi yao ya kwanza aliwaona jinsi walivyosumbua.
“Unajua katika mechi kama hizi ni lazima kabla hamjakutana utafute wachezaji ambao ni nyota kwa wapinzani wako, nilikabidhiwa majina hayo lakini katika mechi hii ya leo (juzi) pia nimemuona mwingine mwenye jezi namba 28 (Singano), naye anaonekana ni mzuri.
“Kama nikipata nafasi ya kusajili, wachezaji hawa ninaweza kuwaongeza katika timu yangu, kwani ni wachezaji wenye kucheza soka vizuri na si sisi, hata timu nyingine nina imani kama zingewaona wangekuwa na wazo kama langu,” alisema.
Akizungumzia mchezo kwa ujumla, alisema walicheza vizuri na kutengeneza nafasi za kufunga, lakini washambuliaji wake hawakuwa makini kukwamisha mpira wavuni ambapo, Simba walitumia vizuri nafasi walizozipata kipindi cha kwanza.
Alisema wamekubali matokeo waliyoyapata, kwani hiyo ni sehemu ya mchezo, hivyo wakati mwingine watajipanga vizuri kuhakikisha wanasonga mbele zaidi.
No comments:
Post a Comment