Baraza la Vijana la Chama cha
Demokrasia na Maendeleo ,CHADEMA, (BAVICHA) mkoa wa Morogoro limesitisha
maandamano ya amani yaliyoandaliwa na Baraza hilo.
Maandamano hayo yalipangwa
kufanyika tarehe 5/3/2012 katika mkoa wa Morogoro.
Madhumuni ya maandamano hayo
yalikuwa kupinga vitendo vya unyanyasaji vinavyofanywa na Jeshi la Polisi dhidi
ya wananchi wasio na hatia na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Maandamano hayo yalikuwa
yafanyike katika wilaya zote za mkoa wa Morogoro na kushirikisha wafuasi wa
CHADEMA, wanaharakati, wasomi pamoja na wananchi wanaoguswa na vitendo vya
unyanyasaji vya jeshi la Polisi.
Lengo kuu lilikuwa kufikisha
ujumbe kwa Serikali na Jeshi la Polisi kiujumla juu ya vitendo hivyo vya unyanyasaji
ambavyo vimekuwa chanzo
cha mauaji ya wananchi wasio
na hatia na hivyo kuhatarisha amani ya nchi.
Hata hivyo,
BAVICHA Mkoa wa Morogoro imeamua kusitisha maandamano hayo kufuatia kikao cha
pamoja kilichofanyika tarehe 2/3/2012 kati ya mkuu wa mkoa wa Morogoro, Mh.
Joel Bendera na viongozi wa BAVICHA mkoa na wilaya ya Morogoro.
Katika kikao hicho
kilichofanyika katika ofisi za mkuu wa mkoa, CHADEMA iliwakilishwa na
mwenyekiti wa BAVICHA Mkoa, Mh. Boniface Ngonyani na mwenyekiti wa BAVICHA
wilaya, Mh. Innocent Zawadi.
Kikao hicho kilifuatia wito
wa mkuu wa mkoa wa Morogoro, Joel Bendera kukutana na viongozi hao kwa lengo la
kujadiliana juu ya mambo mbalimbali kabla ya maandamano hayo kufanyika.
Hata hivyo, katika kikao
hicho, imekubaliwa kuwa uongozi wa BAVICHA mkoa wa Morogoro uwasilishe kwanza
kwa mkuu wa mkoa kero mbalimbali kwa lengo la kufanyiwa kazi na Serikali ya
mkoa.
Mkuu wa mkoa alieleza kuwa
serikali (kwa ujumla) haijashindwa kutatua kero zinazolalamikiwa na BAVICHA hivyo
ni busara zikawasilishwa kwake kwanza ili ziweze kufanyiwa kazi.
Hivyo, imekubaliwa kuwa
viongozi wa BAVICHA mkoa wa Morogoro watakutana tena na mkuu huyo wa mkoa
tarehe 8/3/2012, saa 4.00 Asubuhi katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa
mkoa wa Morogoro kwa lengo la kuwasilisha kero hizo.
TAHADHARI:
BAVICHA mkoa wa Morogoro
imekubaliana na maombi ya mkuu wa mkoa ya kutaka kusitishwa kwa maandamano hayo
na kuwasilishiwa kero mbalimbali kwa njia aliyoona inafaa na hivyo kutangaza
rasmi kusitisha maandamano ya tarehe 5/3/2012.
Hata hivyo,
BAVICHA inapenda kutoa tahadhari kwa mkuu wa mkoa wa Morogoro (Serikali ya
mkoa) kushughulikia ipasavyo kero mbalimbali za kijamii zitakazowakilishwa
kwake.
Iwapo itashindikana, BAVICHA
itafufua upya mpango wake wa kuandaa maandamano makubwa na ya amani mkoani
Morogoro hadi pale kero hizo zitakapopatiwa ufumbuzi.
Aidha, BAVICHA inatoa wito
kwa wafuasi wa CHADEMA mkoa wa Morogoro kuwa watulivu baada ya kusitishwa kwa
maandamano hayo na kwamba kila hatua ya mazungumzo kati ya mkuu wa mkoa na
viongozi wao watajulishwa.
MWENYEKITI BAVICHA MKOA MOROGORO
BONIFACE NGONYANI
************
No comments:
Post a Comment