06 February 2012

Wacheza filamu, Wanamuziki kukamuana leo U/Taifa

TIMU za wasanii wa filamu nchini Bongo Movie FC na timu ya wanamuziki wa bendi 'Kadansi FC' leo zinatarajia kuumana katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ambayo ni maalumu kwa ajili ya kuchangia waathirika wa mafuriko yaliyokea mwishoni mwa wiki.

Katika mechi hiyo mashabiki wa soka watashuhudia wanamuziki na wacheza filamu maarufu wanaotamba hapa nchini.

Wasanii hao juzi walifanya ziara katika eneo la Mwabepande ambako waathirika hao wamehamishiwa kwa ajili ya kujua mahitaji wanayoyahitaji.

Akizungumza katika ziara hiyo, Msemaji wa Kampuni ya Compact Media ambayo ndiyo iliyoandaa Mechi hiyo, Kiason Samweli alisema kwa ujumla wasanii hao wamesikitishwa na maafa hayo.

Alisema watu waliohamishwa sehemu za mabondeni na kupelekwa Mwabepande ni kati ya mashabiki na wapenzi wa filamu mbalimbali wanazozitoa wasannii hao.

Msemaji huyo alisema ziara hiyo ilikuwa maalumu kwa ajili ya kutaka kujua mahitaji ambayo, wanatakiwa kupeleka kwa ajili ya kutoa msaada kwa waathirika hao.

Samweli alisema baada ya mchezo wa leo wanatarajia kukaa kwa siku tatu kwa ajili ya kununua mahitaji mbalimbali yanayohitajika, ili waweze kuwapelekea.

“Tumeguswa sana na suala la mafuriko lililotokea katika maeneo mbalimbali Dar es Salaam, hivyo tumeamua kuandaa mchezo wa hisani kwa ajili ya kuchangisha fedha kwa waathirika waliokumbwa na mafuriko hayo,” alisema.

Naye Mratibu wa shughuli za Uhamishaji Wakazi wa Mabondeni, Gaudence Nyamwihura alisema wamefurahishwa na ziara hiyo ya wasanii hao.

Alisema mahitaji mbalimbali yanahitajika ikiwa ni pamoja na vifaa vya ujenzi na majiko ya mkaa.

“Tumefurahi mno kutembelewa na wasanii leo, ambao ni mfano wa kuigwa na watu wengine kwani kutembelewa tu bila msaada pia ni jambo la busara, hapa kuna nyumba 556, hivyo kuna mahitaji mbalimbali yanayotakiwa hasa vifaa vya ujenzi na majiko ya mkaa kwa kuwa nyumba nyingi wanatumia kuni kupika,” alisema.



No comments:

Post a Comment