16 February 2012

Serikali iwajibike kwa walipa kodi wake

Mhariri Majira,

NAPENDA kutoa dukuduku langu kuhusu hali ya mambo  inavyoendelea hivi sasa nchini.
Nataka nitoe kero kuhusu ucheleweshaji wa kupatiwa ufumbuzi wa matatizo yanayojitokeza ikiwemo mgomo wa madaktari uliomalizika hivi karibuni.

Serikali itambue kwamba, wananchi tunalipa kodi kama kawaida na kila mwezi , tukikatwa katika mishahara kwa lazima bila kujali unalipwa kiasi gani.

Madaktari walilazimika kugoma ili kudai stahili zao, na kuboreshewa mazingira ya kazi ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.

Kwa nini serikali inashindwa kuwalipa wakati inakusanya kodi kama kawaida? Fedha wanazokusanya wanapeleka wapi?

Hakuna asiyejua umuhimu wa kazi ya daktari na ugumu wa kazi yao, nilitegemea  kwamba, daktari ndiye angekuwa  analipwa vizuri kuliko watu wenye fani nyingine kutokana na ugumu na umuhimu wake.  Lakini cha ajabu mwanasiasa hulipwa vizuri kuliko wengine.

Ni lazima serikali iwajibike kwa wananchi kutokana na matatizo yanayoendelea nchini sasa kwa kuwa, lawama zimekuwa zikipelekwa kwa walalamikaji  wakati sio kweli.

Wananchi tumechoshwa na maneno ya kutupoza maumivu yanayotolewa na viongozi huku huduma za jamii zikiendelea kudorora kila kukicha.

Huduma zote ikiwemo elimu, afya,  miundombinu, maji na umeme haziendeshwi inavyotakiwa, huku ikiwa ni haki ya msingi kwa kila mwanachi kuzipata kwa sababu tunalipa kodi.

Wananchi tusidanganyike, tuendelee kudai haki zetu , ni lazima serikali ijifunze kuwajibika kwa walipa kodi.

Mwananchi mwenye uchungu na nchi
Uyole, Mbeya


No comments:

Post a Comment