VIONGOZI wa mahakama nchini wakiwemo Majaji na Mahakimu
wametakiwa kuepuka vitendo vya rushwa na kuhakikisha wanatenda haki pasipo kuangalia sura,uwezo wala kipato cha mtu.
Wito huo ulitolewa juzi na viongozi wa dini mkoani Kilimanjaro wakati wa maadhimisho ya siku ya sheria iliyokuwa na kauli mbiu isemayo adhabu mbadala katika kesi za jinai,faida zake katika jamii.
Viongozi hao walipopewa nafasi ya kufanya maombi kwa ajili ya siku hiyo walisema adhabu mbadala ni muhimu sana lakini pia wahusika wa mahakama wanatakiwa kutenda haki kwa wale wote wanaofikishwa mahakamani.
Akizungumza askofu wa kanisa la Assemlies Of God (TAG), Bw. Glorious Shoo alisema, kumekuwepo na maneno ya kuwepo kwa vitendo vya rushwa mahakamani hali ambayo huonekana kuwakandamiza wananchi wa chini hivyo wahusika ni lazima wahakikishe wanaepuka mambo hayo na kutenda haki.
“Ndugu zangu majaji na mahakimu naomba niwaambie kwamba hakuna kitu ambacho Mungu anapenda kama haki,na siku zote haki isipotendeka amani nayo inatoweka,angalieni maamuzi mnayoyatoa msiwe mnatoa yasiyo ya haki,”alisema Bw. Shoo.
Akizungumza Kaimu Shekhe wa Mkoa wa Kilimanjaro, Bw. Ally Mohamed alisema ni vema majaji na mahakimu wakisimama imara katika kutenda haki bila kuangalia dini,sura wala uwezo wa mtu kwani kufanya hivyo ni kinyume cha maadili.
Naye Mchungaji Albert Mongi wa kanisa la Kiinjili la Kiluther Tanzania aliyekuwepo kwa niaba ya askofu wa kanisa hilo dayosisi ya Kaskazini Dkt. Martin Shao alisisitizia suala la haki katika mahakama na kuongeza kuwa endapo haki itatendeka lawama na manung’uniko kutoka kwa wananchi juu ya viongozi wa mahakama yatapungua.
Kwa upande wake mwakilishi wa askofu wa kanisa Katholiki Jimbo la Moshi Isaac Aman alisema viongozi wa dini wananafasi kubwa ya kuwalea wananchi katika misingi ya sheria hivyo kupunguza idadi ya kesi na watuhumiwa mahakamani.
Alisema pamoja na kazi hiyo kubwa ya viongozi wa dini pia viongozi wa mahakama wanatakiwa kuondokana na vitendo vya rushwa pamoja na tamaa ya fedha ambayo inaweza kuwasababishia kutoa maamuzi yasiyo na haki.
Mapema akizungumza Jaji mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Moshi Bi. Stella Mugasha alisema adhabu mbadala katika kesi za jinai zinafaida kubwa ikiwa ni pamoja na kupunguza msongamano katika magereza na kupunguza gharama za serikali kutokana na kwamba Gharama ya kulisha mfungwa mmoja kwa siku ni shilingi. 2,776.56 gharama ambayo inatokana na bajeti ya Taifa.
Alisema pia wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa elimu na uelewa stahiki kwa jamii na watekelezaji wa sheria husika pamoja na upelelezi wa kesi za jinai kutokamilika mapema hivyo kusababisha mashtaka kukwama.
No comments:
Post a Comment