06 February 2012

Fanyeni kazi kwa kuzingatia Ilani ya CCM- RC

MKUU wa Mkoa wa Shinyanga, Bw. Ally Rufunga amemwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu Bi. Upendo Sanga awapatie wataalamu wake wote nakala moja moja ya Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ili waweze kufanya kazi zao kwa kuzingatia ilani hiyo.


Bw. Rufunga alisema ni muhimu kwa wataalamu na watendaji wengine wote katika halmashauri za wilaya wakatimiza wajibu wao wa kufanya kazi kwa kuzingatia maelekezo yote yaliyomo ndani ya ilani hiyo ya uchaguzi kwa vile CCM ndiyo chama chenye ridhaa ya kuisimamia serikali kwa kipindi hiki cha miaka mitano 2010/2015.

Akizungumza katika kikao cha Baraza la madiwani kilichofanyika juzi mjini Mwanhuzi Meatu, Bw. Rufunga alisema kuanzia sasa kila mtaalamu au mtendaji ye yote ndani ya halmashauri anapaswa kupewa nakala moja ya ilani hiyo ya uchaguzi hata kama atakuwa hana mapenzi na CCM, lakini ni muhimu akatekeleza yale yaliyomo ndani na si
vinginevyo.

“CCM ndiyo iliyokabidhiwa ridhaa ya kuongoza nchi kwa kipindi cha
miaka mitano, kwa hali hiyo sera na ilani yake ya uchaguzi ndivyo vinavyofanya kazi hivi sasa, sera na ilani za vyama vingine vyote vya upinzani hazina nafasi hiyo kwa sasa, vimehifadhiwa makabatini mpaka mwaka 2015.

“Kutokana na hali hiyo, nakuagiza Mkurugenzi kanunue ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 na mpatie kila mtumishi katika halmashauri yako, na kila mtumishi ahakikishe anatekeleza ilani hiyo, na kwa yule anayeona kichefuchefu kwa rangi ya CCM, basi aweke jalada juu yake ili rangi hiyo isimkere, lakini atekeleze yaliyomo,” alisema.

Alisema wapo baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa ambao wamekuwa wakipingana na sera za CCM kitu ambacho kwa hivi sasa hakina nafasi kutokana na kwamba sera hizo ndizo zinazopaswa kutekelezwa baada ya kupewa ridhaa na wananchi kupitia sanduku la kura.

“Ilani na sera ya CCM inaeleza wazi umuhimu wa wananchi  kuchangia miradi ya maendeleo, lakini zipo sera za vyama vingine zinazuia wananchi wasichangie miradi hiyo, si vizuri, kila mmoja anapaswa kutimiza wajibu wake katika suala zima la maendeleo,”

“Wapo wahisani wakiona jamii yenyewe haichangii chochote katika miradi yao ya maendeleo basi na wao wanaondoa ufadhili wao. Tusimamie michango kuhakikisha wananchi wanachangia maendeleo, mkisema kila kitu kitatekelezwa na serikali tutakwama,” alisema.

Kwa upande mwingine mkuu huyo wa mkoa alisema yeye binafsi hana ugomvi na madiwani,lakini ni muhimu wakawahimiza wananchi wao juu ya suala zima la uchangiaji wa miradi ya maendeleo japokuwa ni wazi watachukiwa na wapiga kura kwa hatua hiyo.

No comments:

Post a Comment