03 February 2012

DC aagiza ujenzi wa madarasa ukamilike

Na Jovither Kaijage, Mwanza

BARAZA la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza limeagizwa
kuhakikisha ujenzi wa vyumba 16 vya madarasa vinakamilika ili vitumike kupokea wanafunzi 640 waliofaulu kwenda sekondari na kubaki nyumbani kwa kukosa madarasa mwaka huu.

Agizo hilo lilitolewa jana na Mkuu wa wilaya hiyo, Bi.Queen Mlozi katika kikao cha kawaida cha baraza hilo ambacho kilifanyikia wilayani hapo.

Alisema, tayari Serikali imetoa sh.milioni 128 kwa ajili ya kujenga vyumba 16 vya madarasa katika shule za sekondari 16 ambazo ni za kata na kutaka hadi kufikia mwisho wa mwezi huu madarasa hayo yawe yamekamilika.

Mkuu huyo alisema, katika kukabiliana na tatizo hilo kwa sasa wamefanikiwa  kuhamasisha wananchi ambapo zinajengwa sekondari katika kata mbili za Bukiko na Nyamanga kisiwani Ukara ikiwa ni juhudi zinazolenga kukabiliana na tatizo hilo linalotokea kila mwaka.

Hata hivyo alisema, fedha hizo zilizotolewa na Serikali ambazo kila chumba kimoja cha darasa kimetengewa sh.milioni nane hazitoshi kukamilisha ujenzi huo na kutaka wananchi waongeze nguvu zao.

Alisema, kukamilika kwa shule hizo mbili kutakifanya Kisiwa cha Ukara kuwa na
sekondari tatu hali ambayo itawawezesha wanafunzi wa kisiwa hicho chenye kata nne kupata shule za kutosha hivyo kupunguza wanafunzi wengi kujirundika katika shule 20 zilizopo katika wilaya  hiyo kwa sasa.

Naye mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Bw.Joseph Mkundi alisema, ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule za sekondari za kata ndani ya wilaya hiyo liwe endelevu tofauti na sasa ambapo ujenzi ufanyika baada ya wanafunzi kubaki nyumbani kwa kukosa madarasa ya kuwapokea.

Alisema, tatizo hilo pia lilijitokeza mwaka jana ambapo wanafunzi 1,662 walichelewa kujiunga sekondari na sasa mwaka huu wanafunzi 640 pia wanatarajia kuanza kidatao cha kwanza mwezi Machi mwaka huu baada ya vyumba hivyo vya madarasa kukamilika.

No comments:

Post a Comment