24 January 2012

Ushirika washauri kushiriki katiba mpya

Na Heckton Chuwa,
Moshi

WADAU wa sekta ya ushirika nchini, wameshauriwa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa katiba mpya hatua itayochangia kutoa maoni yao kuhusu masuala ya ushirika 


Ushauri huo umetolewa na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ushirika na Biashara, (MUCCoBS), kilichopo mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro, Prof. Faustine Bee, wakati akifungua semina maalum kwa ajili ya vyama vya ushirika vya akiba na mikopo, (SACCOS), vyenye mitaji
mikubwa,  mwishoni mwa wiki na kuandaliwa na Mungano wa Vyama vya Akiba na Mikopo nchini, (SCCULT).

“Sekta ya ushirika ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi na watu wake, hivyo basi ni muhimu kutumia fursa hii kwa kushiriki mchakato wa katiba mpya  ili ushirika nao uwe na nafasi yake katika katiba mpya ya nchi”, alisema.

Kuhusu maendeleo ya Saccos nchini, Prof. Bee alisema dalili zinaonyesha kuwa zina fanya kazi vizuri na kwamba bado juhudi zinahitajika ili kuziimarisha
zaidi.

“SACCOS  nyingi zinaonekana kuanzishwa ili zipate mikopo kama ile ya mfuko wa Rais Jakaya Kikwete au taasisi zingine za kifedha, si vibaya kuchukua mikopo ila ni vyema uanzishwaji wa SACCOS ulenge zaidi kupunguza umasikini na kuleta maendeleo," aliongeza.

Aidha alitoa mwito kwa SACCOS nchini kuwajengea wanachama wake uwezo wa ujasiriamali na pia kuanzisha miradi yenye tija kwa mfano uanzishwaji wa viwanda vya
kuongeza dhamani ya mazao yanayozalishwa mashambani.

Akizungumza  katika semina hiyo, Mwenyekiti SCCULT,
Bw. Ambrose Shayo, alisema kuwa idadi ya wanachama wake imeongezeka kutoka 205 mwaka 1992 hadi kufikia 1,217 mwaka 2011.

“Ili kusogeza huduma karibu zaidi kwa walengwa wake,
SCCULT tayari imefungua ofisi zake katika mikoa 19 ya Tanzania Bara na pia imeanzisha huduma mpya ambazo zimesaidia taasisi zingine kufahamu umuhimu wa
SACCOS  katika maendeleo ya nchi,” alisema.

Kwa upande wake, meneja wa SCCULT mkoani Kilimanjaro, Bw. Godrick Natai, alisema kuwa kati ya SACCOS 240 zilizosajiliwa mkoani humo ni SACCOS 68 tu ambazo ni
wanachama wa SCCULT.

No comments:

Post a Comment