Na Mwandishi Wetu, Mwanga
WANANCHI wilayani Mwanga Mkoa wa Kilimanjaro wametakiwa kulinda na kutunza
miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa misaada ya wahisani na Serikali kwa
lengo la kuharakisha maendeleo.
Mwito huo ulitolewa kutokana na kuwapo kwa baadhi ya watu ambao siyo waaminifu ambao licha ya kuharibu pia huwa wanaiba vifaa vya miradi ikiwemo umeme wa nishati ya jua.
Rai hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Bw.willy Njau wakati alipotembelea na kukabidhiwa miradi ya utengenezaji wa majiko banifu na umeme wa nishati ya jua katika zahanati na shule za sekondari wilayani humo.
Alisema, suala la utunzaji wa mazingira ni muhimu na kwamba majiko hayo yanasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza uharibifu wa mazingira yatokanayo na kukata miti ovyo.
Alisema, ni vema wananchi wakatumia vizuri misaada inayotolewa na wafadhili
na kuilinda kwa kuwa lengo lake ni huduma muhimu nishati ya umeme hazijafika kuhakikisha wanananchi wanapata huduma bora hususani maeneo ya vijijini ambapo bado.
“Wananchi nawaombeni mtunze miradi mnayokabidhiwa na wafadhili kwani ni kwa
faida yenu na vizazi vijavyo, na kwa kufanya hivyo mtaweza kukua
kimaendeleo kupitia miradi mnayokabidhiwa,”alisema Bw. Njau.
Awali akikabidhi misaada hiyo Mkurugenzi wa shirika lisilo la Kiserikali
la Nishati Endelevu na Utunzaji wa Mazingira (TaTEDO), Bw. Estomih Sawe
alisema, lengo la miradi hiyo ni kuhakikisha wanaleta mabadiliko katika
jamii hususani vijijini na kutunza mazingira kwa kupanda miti kwa kuwa
majiko hayo yanatumia kuni kidogo ikilinganishwa na majiko ya mafiga
matatu.
Naye Meneja wa Nishati na Mazingira TaTEDO, Bi.Gisela Ngoo alisema, ujenzi
wa majiko banifu katika ngazi za kaya utapunguza hewa ya ukaa inayotokana
na matumizi ya kuni na kwamba mpaka sasa jumla ya majiko banifu 1,000
yamejengwa na lengo ni kujenga majiko 10,000.
No comments:
Post a Comment