Na Florah Temba, Moshi Vijijini
IDADI ya wagonjwa wanaofariki dunia katika Hospitali ya TPC
kutoka katika
vijiji jirani vya Mikocheni, Magadini na Chemchem Wilaya ya Moshi
Vijijijni mkoani Kilimanjaro inazidi kuongezeka mara kwa mara kutokana
na kukosekana kwa huduma za afya katika vijiji hivyo.
Hayo yalibainishwa mwishoni mwa wiki na Ofisa Utawala Mkuu wa Kampuni ya TPC Bw.Jafary Ally ambapo alisema, wagonjwa hao huwa wanafika katika hospitali hiyo wakiwa katika hali mbaya kutokana na maeneo hayo kutokuwa na vituo vya afya na vyombo vya usafiri.
Alisema, pamoja na kukosekana kwa vituo hivyo na vyombo vya usafiri pia
kuna umbali mrefu kufika katika hospitali hiyo ili kupata huduma hususani akina mama wajawazito.
Alisema, kutokana na kukosekana kwa vyombo vya usafiri wagonjwa hao
hulazimika kusafirishwa kwa kutumia baiskeli na mikokoteni hadi hospitalini hapo hali ambayo aliishauri halimashauri ya wilaya hiyo kuangalia uwezekano wa kupeleka huduma za afya na wataalamu ili kuokoa maisha ya wananchi hao.
“Vijiji vinavyozunguka hospitali hii, havina vituo vya afya na kutokana na
hali hiyo wananchi wa maeneo haya wanalazimika kuja kupata matibabu katika
hospitali yetu ya TPC,”alisema Bw.Jafari.
Naye Diwani wa Kata ya TPC, Bw.Rojas Mmari alisema, kata hiyo ina zahanati moja ambayo haina madakatari wala dawa na kusema kuwa nyakati za mvua hali inakuwa mbaya zaidi kutoka na wananchi kushindwa kutoka kwenda kutafuta huduma ya afya kutokana na hali ya mazingira yalivyo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Chemchem, Karebia Malekule alisema,
hali ya upatikanaji wa huduma za afya ni mbaya hususani kipindi cha mvua za
masika kutokana na miundombinu ya barabara kuwa mibovu na dawa kutofika kwa
wakati katika kijiji hicho.
No comments:
Post a Comment