Na Zahoro Mlanzi
SIKU moja baada ya timu ya African Lyon kulituhumu Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
juu ya suala la Yusuph Soka, shirikisho hilo limeibuka na kusema wanabebeshwa mzigo ambao sio wa kwao.
Mbali na hilo, shirikisho hilo limekubali kuyafanyia kazi maombi ya timu hiyo juu ya kupangwa vibaya kwa baadhi ya mechi zao za Ligi Kuu Bara na kwamba suala hilo litafikisha kwa Kamati ya ligi hiyo.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa shirikisho hilo, Boniface Wambura alisema wanashangaa kwanini wao wanahusika na suala la Soka kudaiwa kukamatwa na dawa za kulevya nchini Swiden.
"Unajua suala kama hilo ni kosa la jinai, sasa sisi TFF tunaingizwaje katika hilo ni sawa na lile la mabondia waliokamatwa Mauritius ambapo baada ya uchunguzi wakakamatwa waliohusika na tukio lile," alisema Wambura.
Alisema hawakutoa ITC (Hati ya Uhamisho ya Kimataifa) ila walichofanya baada ya kuitaka Lyon na Soka wamalize tofauti zao, walimpa barua ya kumruhusu akafanye majaribio na si vinginevyo.
Akilitolea zaidi ufafanuzi suala hilo, alisema Soka alikuwa na mgogoro na Lyon ambapo mgogoro huo ulifika mpaka kwa Kamati ya Sheria, Hadhi na baada ya kamati hiyo kulijadili kwa kina ikabaini mchezaji huyo ana kosa na akatakiwa aombe msamaha.
Alisema baada ya kuamliwa hivyo aliomba msamaha na Lyon wakaiambia TFF kwamba wameshamalizana naye na ndio maana wakakubali aende kufanya majaribio huko Swiden.
Aliongeza, kama baada ya kwenda huko amekamatwa na dawa za kulevya, hilo wao haliwaruhusu ila kama kweli amekutwa nazo anadhani anaweza kuchukuliwa hatua kwa sheria za huko.
Mbali na hilo, akizungumzia malalamiko ya timu hiyo katika ratiba, alisema kweli hilo wameliona na linashughulikiwa ambapo mechi zinazoonekana zina utata zinaweza kuingizwa Aprili ndio mwezi unaonekana ratiba imekaa vizuri.
No comments:
Post a Comment