16 December 2011

Yanga yapata dawa ya Zamalek

Na Zahoro Mlanzi

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga inatarajia kujipima na timu sita kutoka nchi mbalimbali za Afrika, ili kujiweka fiti na mechi ya
Klabu Bingwa Afrika dhidi ya Zamalek.

Timu hiyo imepanga kucheza na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC), Bunamwaya ya Uganda, SOFAPAKA ya Kenya na Mamlaka ya Mapato ya Uganda (URA) ili kujiweka sawa na ligi hiyo na mechi ya Klabu Bingwa Afrika dhidi ya Zamalek ya Misri.

Mbali na timu hizo, pia zimo Telecom ya Burundi, Power Dynamo ya Zambia pamoja na Kombe la Mapinduzi ambapo mechi hizo zitatosha kuwaweka fiti na mzungo wa pili wa ligi hiyo na mechi dhidi ya Zamalek.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Louis Sendeu alisema mazungumzo ya mechi hizo, yanaendelea kadri siku zinavyosonga mbele, kwani wanahitaji mechi nyingi zaidi za kimataifa, ili kujiandaa vizuri na mashindano mbalimbali.

“Kocha Papic (Kostadin), anahitaji mechi kama sita hivi za kimataifa na tayari tumeshaanza mazungumzo na timu za TP Mazembe ambayo yanaendelea vizuri, Bunamwaya, URA, TELECOM ya Burundi, Sofapaka na Power Dynamo ya Zambia na tuna imani kila kitu kitakwenda sawa,” alisema Sendeu.

Alisema mechi hizo, pamoja na mashindano ya Kombe la Mapinduzi ambayo yataanza mwezi ujao Zanzibar, zitawasaidia kujiandaa dhidi ya Zamaleki ambayo inaonekana kuteka hisia za mashabiki wa soka nchini.

Sendeu alisema kuitoa timu hiyo hakuitaji uchawi, ila ni kujiandaa vizuri na wanajua ina wachezaji wazuri kama Ahmed Hassan 'Mido' na Amr Zakhi ambapo kwa nyakati tofauti wamecheza ligi mbalimbali za Ulaya ikiwemo Ligi Kuu Uingereza, hivyo maandalizi mazuri ndiyo mkombozi wao.

Mbali na hilo, pia alizungumzia kuhusu wachezaji Hamis Kiiza 'Diego' na Haruna Niyonzima 'Fabregas', kujiunga na wenzao baada ya kupewa likizo ya siku tatu, alisema walitarajia jana jioni kurudi nchini na mshambuliaji, Davies Mwape aliyeumia nyama za paja anaendelea vizuri kwa kufanya mazoezi mepesi.

Pia alizungumzia suala la kupiga kambi nje ya nchi ambapo, alisema kwa sasa uongozi haujapanga timu hiyo itaweka kambi wapi, lakini baada ya kumaliza mechi zao za kimataifa na Kombe la Mapinduzi kama kuna haja ya kufanya hivyo wataweka wazi.


No comments:

Post a Comment