Na Mwandishi Wetu, Dodoma
JESHI la Polisi Mkoa wa Dodoma, limekiri kuzuka kwa wizi wa magari unaofanywa na watu wanaosadikiwa kuwa wezi kutoka Mkoa wa Arusha na kuwataka wananchi kuwa
makini na vyombo hivyo.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi juzi, Mkuu wa Upelelezi wa makosa ya jinai Mkoa wa Dodoma (RCO) Polcarp Urio, alisema tayari amepokea taarifa za kuzuka wizi wa magari mkoani humo na kwamba wanaifanyia kazi.
Wezi hao wanadaiwa kuiba magari mawili yakiwa yameegeshwa nje ya Ofisi za Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) na moja likiwa eneo la chako ni chako mjini hapa kwa kutumia funguo maalum (Master key).
Bw. Urio aliwataka wananchi kuchukua taadhari kwa kuepuka kuamini zaidi milango ya magari yao pekee na kutokuacha vitu vya thamani ndani ya vyombo hivyo.
Alisema wezi hao wanadaiwa kuwa na gesi maalum ya kukata vioo vya magari na kwamba iwapo mtu akiacha kitu chenye thamani wanaweza kuutumia kufanikisha wizi wao.
Alisema polisi haliwezi kutaja namba za magari zilizoibiwa kwa sasa kwa kuwa kunaweza kuharibu upelelezi.
No comments:
Post a Comment