Na Salim Nyomolelo
*Prof. Mukandala atoa onyo kwa wengine waliobaki
CHUO Kikuu cha Dar es Salaam Kampasi ya Mlimani, kimefukuza na kuwafutia udahili wanafunzi 43 kwa kosa la kufanya vitendo vya uhalifu vilivyosababisha uvunjifu wa amani chuoni hapo na kuvuruga shughuli za taaluma na utawala.
Akitangaza uamuzi huo kwa waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Rwekaza Mukandala, alisema hatua hiyo inalenga kuondoa vitendo vya uhalifu chuoni hapo.
Alisema vitendo vya uhalifu vilivyofanywa na wanafunzi hao ni pamoja mna kuingia darasani na kuwacharaza fimbo wenzao waliokuwa wakisoma na kuwazuia wasiendelee na masomo na kuwamwagia maji waadhiri.
Aliongeza kuwa, uhalifu mwingine ni kuziba njia ya kuelekea jengo la utawala hivyo kusimamisha shughuli za chuo na kumwaga chakula kwa wenzao waliokuwa wakiendelea na masomo.
“Kutokana na ongezeko la vitendo vya uhalifu na uvunjifu wa amani, Desemba 13, 2011, Kamati ya Wakuu wa Koleji na shule, ilifanya kikao cha dharura na kutoa mapendekezo ya hatua za kuchukua ili kukomesha uhalifu chuoni.
“Jioni ya siku hiyo, Baraza la Chuo nalo lilifanya kikao cha dharura ili kutathmini mwelekao wa chuo katika kipindi kifupi kilichopita pamoja na kupitia mapendekezo yaliyotolewa na Kamati ya Wakuu wa Koleji na shule na kutoa maamuzi haya,” alisema.
Alisema wanafunzi nane waliokuwa wamesimashiwa masomo kwa miezi tisa na wengine ambao walisimamishwa kwa muda wakisubiri kumalizika kwa kesi zao mahakamni pamoja na viongozi wa vurugu zilizotokea Desemba 12-13 mwaka huu, iliamuliwa wafukuzwe chuo mara moja.
Aliongeza kuwa, mwanafunzi yeyote ambaye atafanya kitendo chochote cha uhalifu pamoja na kuwatisha wenzake au kufanya mkutano nje ya taratibu za chuo, achukuliwe hatua kama hiyo.
Prof. Mukandala aliongeza kuwa, pia kikao hicho kiliagiza kuwepo na ulinzi wa kutosha katika maeneo yote muhimu ya chuo ili wanafunzi waweze kuendelea na masomo kama kawaida.
“Baraza limeagiza mawasiliano yafanyike kwa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HELSB) na Tume ya Vyuo Vikuu (TCU), ili wanafunzi waliofukuzwa kutokana na uhalifu wasipewe mkopo tena na Serikali wala kuruhusiwa kusoma katika chuo chochote cha umma,” alisema.
Alisema baraza pia limeagiza wanafunzi wanaoendelea na masomo, wazazi wao na wafanyakazi wajulishwe kuhusu hatua za usalama zinazochukuliwa ili kuweka eneo hilo katika hali nya amani.
Alisema madai ya wanafunzi waliofanya mgomo chuoni hapo yalikuwa yakibadilika mara kwa mara hivyo kusababisha uongozi wa chuo kufanya uchunguzi wa kina kama wanafunzi hao wana nia ya kweli na masomo au la.
Prof. Mukandala alisema awali walidai mikopo kwa ajili wanafunzi waliochaguliwa bila kupatiwa fedha hizo na baadaye kudai wenzao waliokamatwa na polisi kwa kuendesha maandamano kinyume cha sheria waachiwe huru.
Alisema hivi karibuni wanafunzi hao walitaka kuondolewa adhabu za utovu wa nidhamu dhidi ya wenzao wachache lakini baadaye wakageukia suala la kupatiwa fedha za malazi na chakula kwa kipindi cha kuanzia Desemba 10 mwaka huu.
“Jambo kubwa lililojitokeza ni kwamba, madai haya yalikuwa tayari yametatuliwa na chuo kwa kushirikisha uongozi halali wa wanafunzi chuoni hapa (DARUSO) lakini kundi dogo la wanafunzi pia lilitangaza kupindua Serikali halali ya wanafunzi hivyo kusababisha kuvunjwa mlango wa mmoja wa ofisi za viongozi hawa.
“Utawala wa chuo unawasihi wanafunzi na wafanyakazi wote kuendelea na shughuli zao bila wasiwasi wowote,” alisema.
No comments:
Post a Comment