15 December 2011

Tutatoa uamuzi maombi ya TANESCO Januari-EWURA

Na Rachel Balama

BODI ya Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) inavuta pumzi kutoa uamuzi wa kukataa au kuridhia kupanda kwa bei za umeme kama ilivyoombwa na Shirika la Umeme nchini TANESCO.
Bodi hiyo ya EWURA imepanga kukutana Desemba 15 na 16, mwaka huu kujadili na kutoa uamuzi juu ya mapendekezo hayo ya TANESCO pamoja na maoni yaliyotolewa na wadau wa huduma hiyo mwezi Januari mwakani.

Akizungunza na mwandishi wa haabri hizi, Ofisa Habari wa EWURA Bw. Titus Kaguo, alisema baada ya bodi hiyo kukutana kujadili mamlaka hiyo itatoa taarifa kamili mwezi Januari mwakani.

Hata hivyo wananchi walionyesha wazi kutounga mkono maoni hayo ya TANESCO kwa sababu mbalimbali.

Baadhi ya sababu zinazotajwa na wananchi kukataa maombi hayo ni kusuasua kwa uapatikanaji wa umeme wenyewe, kupanda kwa gharama za maisha, bei kubwa ya kuunganisha huduma hiyo pamoja na sababu nyingine nyingi.

Wakati EWURA ikivuta pumzi kutoa uamuzi wake TANESCO limesema linasubiri kwa hamu maamuzi hayo na kwamba haliwezi kuzungumza lolote kwa sasa kuhusu maombi ya kupandisha gharama za umeme kwa kuwa hawajajibiwa rasmi.

TANESCO iliomba kupandisha bei za umeme kwa  wastani kutoka sh. 141 ya sasa kwa unit hadi sh. 359 ifikapo Januari mwakani.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu jana Ofisa Uhusiano wa TANESCO, Bi. Badra Masoud, alisema wanasubiri majibu ndio wapate cha kuzungunza.

"EWURA ndio wanaweza kutoa majibu lakini kwa upande wetu sisi hatuwezi kusema chochote kwa kuwa sisi tuliomba," alisema.

No comments:

Post a Comment