07 December 2011

Serikali kuendelea kulinda usalama afya za binadamu

Na Anneth Kagenda

SERIKALI imesema itaendelea kuchukua hatua za makusudi katika kuhakikisha inalinda usalama, afya za binadamu na mazingira ili kuwaepusha na Teknolojia ya mimea
inayojulikana kama Bioteknolojia ya Kisasa ambayo imekuwa ikisababisha uharibifu wa mazingira yao.

Hayo yalisemwa Dar es Salaam jana na Kaimu Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, Bi. Magdalena Mtenga aliyemwakilisha Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Bw. Sazi Salula wakati wa warsha ya wadau kuhusu matumizi salama ya Teknolojia ya mimea.

Alisema kuwa zimekuwapo Teknolojia mbalimbali lakini hii ya mimea ni ya kisasa zaidi na uharibu mazingira, afya za binadamu ambapo wadau, wataalamu wa mazingira wanapaswa kuzitambua vizuri ili  kuinusuru jamii.


Alisema kuwa kutokana na kuwapo kwa changamoto hiyo ofisi yake inaendelea kuandaa miongozo mbalimbali kwa ajili ya usalama wa mazingira dhidi ya athari zinazoweza kutokana na matumizi ya Bioteknolojia hiyo ya kisasa ili kupata uelewa mzuri na kujua matumizi na kusema kuwa kazi ya kuelimisha inahitaji ushirikiano mkubwa wa wadau wote hususan waliohudhuria washa hiyo.

"Upo umuhimu wa kuhakikisha kwamba wadau wote kwa ujumla wao wanaelimishwa na kuelewa vizuri kanuni na miongozo ya usimamizi wa usalama wa mazingira dhidi ya athari za Biotekinolojia ya kisasa na pindi watakapokuwa wameelewa hata jamii itapata uelewa kupitia kwao.

"Hii ni warsha mahususi kwa wadau mbalimbali katika suala hili muhimu la usimamizi wa matumizi salama ya biotekinolojia ya kisasa hapa nchini na tayari serikali imeshafanya jitihada za kuandaa sheria, kanuni, miongozo na taratibu husika za usimamizi wa matumizi yake pamoja na kwamba uelewa ni mdogo, alisema Bi. Mtenga.

Alisema lengo la teknolojia hiyo ni kukidhi haja mbalimbali kama kuimarisha ubora, kudhibiti magonjwa, kuhimili ukame na kukuza uzalishaji na kusema kuwa pamoja na faida za biotekinolojia ya kisasa bado upo wasiwasi kuhusu athari zinazoweza kupatikana kutokana na teknolojia hiyo endapo itatumiwa bila kufuata taratibu za usalama wa wenyewe.

No comments:

Post a Comment