Na Zahoro Mlanzi
KOCHA Mkuu wa timu ya Yanga, Kostadin Papic, ameutaka uongozi wa klabu hiyo kutafuta mechi nyingi za kimataifa, ili iwe na uwezo wa kuiondoa Zamaleki ya Misri, katika michuano ya
Klabu Bingwa Afrika, mwakani.
Timu hiyo imepangwa kuanzia nyumbani na miamba hiyo ya Misri kati ya Februari 17, 18 na 19 mwakani huku watani zao wa jadi, Simba ambao wapo katika Kombe la Shirikisho ikipangwa na Kiyovu Sport ya Rwanda, lakini wao wataanzia ugenini.
Kwa upande wa Zanzibar, Mafunzo itaanzia nyumbani dhidi ya Muculmano de Maputo ya Msumbiji katika michuano ya Klabu Bingwa na Jamhuri, pia wataanzia nyumbani dhidi ya Hwange ya Zimbabwe, mechi zote zinapigwa kati ya tarehe hizo.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Louis Sendeu alisema tayari maandalizi dhidi ya Wamisri hao, yameshaanza na Papic anajipanga kwa ajili ya kuandaa programu maalumu kwa ajili ya kujiandaa na meche hiyo.
"Ni lazima tujiandae vya kutosha na tayari kocha Papic, ameuagiza uongozi ujipange kuhakikisha unatafuta mechi nyingi za kimataifa na kufanya mazoezi ya nguvu, kwani timu hiyo ina historia nzuri katika michuano hiyo," alisema Sendeu.
Alisema ni kweli timu za Kaskazini mwa Afrika, huwa zinawasumbua sana lakini hivi sasa hawatakubali kuendeleza uteja na wanaamini timu hiyo haipo katika kiwango kizuri kwa miaka ya hivi karibuni, ikilinganishwa na miaka ya 1980 na 1990.
Katika hatua nyingine, Sendeu alizungumzia suala la beki wao Godfrey Taita, ambaye aliondolewa katika kambi ya timu ya taifa ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars), kwa utovu wa nidhamu, alisema wanashangazwa kuona mpaka leo hawajapewa taarifa rasmi za tukio hilo.
"Unajua TFF (Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania), huandika barua kuomba mchezaji kujiunga na timu ya taifa, lakini tunapata wasiwasi juu ya tukio la taifa kwani mpaka leo wamekaa kimya, hivyo tunaamini inawezekana Taita hakuwa na kosa," alisema Sendeu.
Alipotafutwa Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura juu ya suala hilo, alisema hata wao hawajapata ripoti rasmi kutoka kwa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Charles Mkwasa lakini watakapoipata hawatosita kuiwasilisha kwa klabu hiyo.
"Si suala la taifa tu, hata sisi pia tunasubiri ripoti ya Boban (Haruna), tuna imani Mkwasa na benchi lake itazileta kwa pamoja ripoti hizo na baada ya hapo mambo mengine yatafuata," alisema Wambura.
No comments:
Post a Comment