16 December 2011

Muhimbili yalia na upungufu madaktari wa moyo

Flora Amon na Surah Mushi

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili imesema ina upungufu mkubwa wa madaktari bingwa wa moyo pamoja na mashine za kupima ugonjwa huo maarufu kama (ECO). Akizungumza na
gazeti hili ofisini kwake jana, Ofisa habari wa hospitali hiyo Bw. Aminiel Aligaesha, alisema kutokana na hali hiyo wagonjwa wanapangiwa muda mrefu kuonana na madaktari hao.

Bw. Aligaesha alikuwa akijibu maswali ya gazeti hili kuhusu sababu za wagonjwa wa moyo kupangiwa muda mrefu kufanyi kipimo hicho.

Awali baadhi ya wagonjwa waliozungumza na Majira walisema walielezwa kuwa wanatakiwa kufanyiwa kipimo cho cha ECO mwakani kutokana na madaktari waliopo kubanwa.

"Niliambiwa kuwa ninaweza kufanyiwa kipimo hicho mwakani hata mwezi wa nne kwa kuwa madaktari wamebanwa na wagonjwa wengi,"alisema mmoja wa wagonjwa.

Ofisa habari huyo alisema kwa sasa Hospitali hiyo ya taifa ina madaktari watatu tu wa moyo ambao wanalazimika kuwapima wagonjwa na kuendesha kliniki pia kwa wagonjwa wa nje.

"Watalaamu wa kupima ugonjwa wa moyo wapo watatu ila kwa sasa mmoja ni mgonjwa, hivyo inachukua muda mrefu mgonjwa kumuona daktari,  wanakuwa na majukumu mawili kwa wakati mmoja kwenda kliniki na kuwapima wagonjwa,"alisema Bw. Aligaesha.

Alisema madaktari hao kwa siku wanawaona  wagonjwa wasiopungua 20 na kwamba kipimo hicho hakipimwi na mtu mwingine tofauti na daktari husika.

Aliwaomba wagonjwa kuwa wavumilivu kutokana na uchache wa wataalamu hao wakati wakiendelea kufanya utaratibu kuongeza wengine na kwamba kitengo hicho bado ni kipya katika hospitali hiyo.

Akizungumzia ubovu wa mashine ya CTscan iliyokuwa imeharibika kwa muda wa mwezi mmoja na nusu mzima na kusababisha usumbufu mkubwa kwa wagonjwa, alisema huduma chombo hicho kimepona tangu jumamosi iliyopita.

Bw. Aligaesha alitaja sababu za mashine hiyo kuchukua muda mrefu kutengenezwa kuwa ni kukosekana kwa vifaa vyake nchini hivyo kuilazimu serikali kuwasiliana na watengenezaji.

"Vifaa vingi vya tiba vinatoka nje ya nchi hivyo ikitokea mashine kuharibika inachukua muda kidogo kupona kutokana na mchakato wa manunuzi kuchukua muda,"alisema Bw. Aligaesha.

Alisema inapotokea hali hiyo wagonjwa wenye hali mbaya hulazimika kwenda katika hospitali binafsi ambazo gharama ni kubwa.

No comments:

Post a Comment