Na Zahoro Mlanzi
RAIS wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein anatarajia kuwa mgeni rasmi, katika sherehe za kufunga michuano ya 35 ya Kombe la Tusker Chalenji,
inayoendelea kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema sherehe za ufungaji wa mashindano hayo, yaliyoshirikisha mataifa 10 wanachama wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) na timu mbili mwalikwa, zitafanyika Jumamosi.
Alisema mara baada ya kumalizika kwa mchezo wa fainali siku hizo, Rais Shein atakabidhi zawadi kwa washindi pamoja na kuyafunga rasmi mashindano hayo.
Wakati huohuo, Wambura alisema aliyekuwa mshambuliaji wa Yanga, Robert Jamal Mba ambaye ni raia wa Cameroon, ameombewa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) ili acheze soka nchini humo.
Alisema Shirikisho la Mpira wa Miguu Cameroon (FECAFOOT), limetuma maombi hayo juzi kwa TFF ili kupata hati hiyo.
Wambura alisema Mba, ambaye aliichezea Yanga enzi za uongozi wa aliyekuwa Mwenyekiti wa wakati huo, Imani Madega ameombewa ITC kwa ajili ya kujiunga na klabu yake ya zamani ya Tiko United, baada ya mkataba wake ndani ya Yanga kumalizika.
Aliongeza kuwa kutokana na hilo, TFF inafanyia kazi maombi hayo na ITC, itatolewa wakati wowote baada ya taratibu husika kukamilika.
No comments:
Post a Comment