06 December 2011

Bil. 1/- zatumika ujenzi kituo cha mafuta cha serikali

Na Rehema Maigala

ZAIDI ya sh. bilioni moja zimetumika katika mradi wa ujenzi wa kituo kipya cha mafuta cha serikali katika eneo la Kurasini,
Dar es Salaam kwa lengo la kuboresha mazingira ya kutolea huduma kwa wateja katika eneo hilo.

Akizungumza katika ufunguzi wa kituo hicho cha mafuta cha serikali jana, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GPSA), Bw. Josephat Mwambega, alisema fedha hizo pia zimetumika kwa ajili ya kuongeza uwezo wa kuhifadhi mafuta.

Alisema awali walikuwa wanahifadhi mafuta lita 108,000 tu lakini sasa wanao uwezo wa kuhifadhi hadi lita 197,000.

Alisema mpangilio wa kituo hicho kwa sasa unaeneo maalumu lenye pampu mbili mahususi kwa ajili ya kutolea mafuta kwa magari ya viongozi ngazi ya Mawaziri, Naibu Waziri, Makatibu Wakuu, Naibu Katibu, Wakuu wa Idara Wizara zinazojitegemea, Wakurugenzi wa Wizara na Wakala za Serikali na Mashirika.

Hata hivyo alisema kwa sasa wastani wa magari yanayohudumiwa na wakala kwa siku za Jumatatu ni magari 800 na kwamba kabla ya kufanya ukarabati huo kazi ilikuwa ngumu hivyo kuwalazimu kufanya kazi hadi usiku.

Bw. Mwambega alitaja changamoto zinazowakabili kuwa ni pamoja na upungufu wa vitendea kazi na kwamba hata vilivyopo navyo ni chakavu kwa kuwa ni vya muda mrefu, majengo ya ofisi na maghala pamoja na ufinyu wa bajeti.

Kituo hicho kilifunguliwa na Waziri wa Fedha, Bw. Mustapha Mkulo, ambaye aliweka mafuta katika gari lake kama ishara ya ufunguzi wa kituo hicho rasmi.

1 comment:

  1. Hongereni sana ni ubunifu mzuri sana.
    Sasa fanyeni kazi kwa nidhamu na uzalendo wa hali ya juu ili serikali ipate faida na kuokoa gharama kubwa za uharibifu wa magari kwa mafuta ya kuchakachuliwa. Kama kituo hiki kitaonyesha ufanisi mkubwa basi viwepo vingine kwenye mikoa maalumu itakayohudumia magari ya serikali sehemu mbalimbali za nchi. Si kwamba tunarudi nyuma bali ni hatua ya kuokoa gharama na uchumi nchi kwani kuna wizi na udanganyifu mkubwa kwenye uwekeaji wa mafuta kwenye magari ya serikali. Hongera sana.

    ReplyDelete