Na Suleiman Abeid, Shinyanga
MKAZI wa Kijiji cha Mwanyahina wilayani Meatu Mkoa wa Shinyanga, aliyetambuliwa kwa
jina la Bi. Kundi Ntalima (50), amekufa baada ya kunywa pombe haramu ya gongo kupita
kiasi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Bw. Diwani Athumani, alisema tukio hilo
lilitokea juzi saa sita usiku katika Kijiji cha Busia wilayani Meatu wakati Bi.
Ntalima akiwa nyumbani kwa mdogo wake aliyetajwa kwa jina la Bi. Liku Mosha.
Kamanda Athumani alisema siku hiyo ya tukio Bi. Mosha alimwachia marehemu nyumbani ili kumwangalizia mji wakati akisafari kwenda wilayani Bukombe na kwamba mtu anayedaiwa kuwa ni muuza gongo maarufu kijijini hapo Bw. Mashalla Sono alipeleka pombe
hiyo haramu na kumuuzia marehemu.
Alisema baadaye Bi. Ntalima alianza kunywa pombe hiyo huku akiwa hajapata chakula cha jioni na kuinywa nyingi kupita kiasi na kusababisha azidiwe kutokana na kukosa chakula mwilini hali iliyosababisha kifo chake baada ya kupoteza fahamu kwa ulevi.
Hata hivyo mtu aliyepeleka pombe hiyo alitoroka baada ya kubaini Bi. Kundi amefariki na hivi sasa anasakwa na polisi ili aweze kufikishwa mahakamani kujibu shitaka la kusababisha kifo hicho.
Katika tukio lingine Jeshi la Polisi linawaaka watu wanaotuhumiwa kuhusika na uporaji pamoja na
kumbaka na kumsababishia maumivu makali mwanamke mmoja mkazi wa Kijiji cha Mwawaza Manispaa ya Shinyanga.
Kamanda Athumani alisema tukio hilo lilitokea Desemba mosi saa 2.00 usiku katika Kijiji cha Mwawaza Manispaa ya Shinyanga baada ya watu hao kuivamia familia ya Bw. Jibushi Madilo (29) walipokuwa nje ya nyumba yao wakipata chakula cha jioni.
Akifafanua tukio hilo Kamanda Athumani alisema baada ya watu hao kufika katika mji huo wa Bw. Madilo walikaribishwa chakula na kukubali kula pamoja ghafla baada ya kumaliza waliwaweka chini ya ulinzi wenyeji wa mji huo huku wakiwalazimisha kutoa fedha.
Alisema katika vurugu hizo watu hao walimkamata mwanamke aliyekuwa akila chakula pamoja na Bw. Madilo na kuingia naye ndanik ambako walimbaka na kumsababishia maumivu makali.
Alisema baada ya kitendo hicho watu hao walipora simu moja aina ya NOKIA yenye thamani ya sh. 50,000, mbegu za mahindi kilo nne zenye thamani ya sh. 10,000, njugumawe pamoja na nguo mbalimbali za watoto.
Alisema katika utekaji huo watu hao walitumia bunduki iliyodaiwa kuhifadhiwa katika mfuko na kwamba polisi walipofika eneo la tukio waliokota risasi moja inayotumika katika bunduki aina ya SMG au SGR.
Kamanda Athumani ametoa wito kwa raia wema kutoa taarifa pale wawaonapo watu wowote
wanaotilia shaka ili waweze kukamatwa na kufikishwa makahamani.
No comments:
Post a Comment