23 November 2011

Magamba CCM hayabanduki

*CC yachemsha, yaachia vikao vya juu

Na Pendo Mtibuche, Dodoma

KIKAO cha Kamati Kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kilichoanza kukutana juzi na jana mjini Dodoma, kimetawaliwa
na kigugumizi, huku wale wanaotakiwa kujivua magamba wakiendelea kubaki.

Katibu wa Halmashauri Kuu, Itikadi na Uenezi, Bw. Nape Nnauye, alisema kuwa baadhi ya mambo yaliyojadiliwa ni lazima yapelekwe kwenye vikao vingine ili yajadiliwe zaidi.

Hadi kufikia muda wa mapumziko kwa ajili ya chakula cha mchana jana, jambo kubwa lililokuwa limejadiliwa ni kuhusu azimio la chama hicho kujitegemea kiuchumi, ili kiache kutegemea ruzuku kutoka serikalini.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya wajumbe wa kikao hicho kupata muda wa mapumziko kwa ajili ya chakula cha mchana jana, Bw.Nnauye alisema suala lililojadiliwa ni la chama kujitegemea kiuchumi.

Alisema kuwa ajenda hiyo ilichukua muda mrefu  kujadiliwa, lengo likiwa ni kukifanya chama kujitegemea na kuacha kutegemea ruzuku toka serikalini.

Hata hivyo alisema kuwa mbali na ajenda hiyo, kujadiliwa kwa kina, lakini kikao hicho lazima kimalize kazi zake hata kama ni usiku wa manane, kwa kuwa ajenda zinazohitajika kujadiliwa bado ni nyingi na mambo ya kuzungumziwa kwenye kikao hicho ni mengi.

"Zipo ajenda nyingi na siwezi kuzitolea taarifa kwa umma, kwani mambo hayo bado yanahitaji kwenda  katika ngazi za juu za vikao vingine ili kuendelea kujadiliwa, hivyo kama kuna uvumi wowote juu ya jambo fulani acha liendelee hivyo, lakini mimi nilichoeleza ndicho, na ni vizuri mkapata taarifa kutoka vyanzo sahihiĆ¢" alisema Nape 

Nape alikuwa akijibu swali lililomtaka aeleze kuhusu taarifa zilizozagaa mtaani kuwa mmoja wa wanasiasa wanaotakiwa kujivua gamba, amefanya hivyo.

Alisisitiza kuwa hali ya kikao hicho ilikwenda vizuri na watakapoingia saa kumi na nusu hawajui watamaliza saa ngapi.

"Lengo letu ni kumaliza mambo yote siku ya leo (jana), ili kesho (leo) kianze kikao cha Halmashauri Kuu," alisema Bw. Nape.

1 comment:

  1. Kazi njema,ila msitufanye wanachama wa ccm kama wabunge walivyotufanya kuyafanya mawazo yao kuwa ni mawazo ya wananchi. Tunataka CCM imara na CHADEMA imara ili tushindane kwa manufaa ya wananchi. Angalia Tigo Airtel, Voda nk

    ReplyDelete