12 October 2011

Warioba: Tanzania itapata matatizo makubwa

Waziri Mkuu Mstaafu, Bw. Joseph Sinde Warioba akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) Dar es Salaam jana baada ya kutembelea maonesho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanganyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja, Kulia ni Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI, Bw. Kassim Majaliwa.

Na Benjamin Masese

WAZIRI Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Warioba ametoa tathmini yake ya miaka 50 ijayo, akisema
Tanzania itakumbwa na matatizo makubwa kutokana na dalili zilizopo katika nyanja za kiuchumi, umeme, bei ya mafuta, kushuka thamani ya fedha na hali ya kisiasa.

Hayo aliyasema Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutembelea mabanda ya Ofisi ya Waziri Mkuu katika maonesho ya maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru wa Tanganyika yanayofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja.

Alisema kuwa matatizo yatakayotokea yatakuwa makubwa kuliko yalitokea wakati wa kupigania uhuru wa Tanganyika na katika kipindi cha uongozi wa Hayati Mwalimu Julius Nyerere, yakichangiwa na baadhi ya viongozi kushindwa kufuata misingi ya waasisi wa taifa badala yake wamekuwa katika malumbano ya kisiasa.

Jaji Warioba alisema mtazamo wake unatokana na hali halisi ilivyo na changamoto zinazolikabili taifa pamoja na viongozi kushindwa kupanga mipando ya maendeleo na kupambana na changamoto, badala yake wamekuwa katika migogoro ya kisiasa.

"Huko mbele tuendako katika miaka 50 ijayo kwa mtazamo wangu, kutakuwa na matatizo makubwa sana kuliko yaliyowahi kutoka katika awamu ya Hayati Nyerere, taifa halitafika salama. Nchi imekuwa ya kisiasa, ushahidi shika magazeti asubuhi asilimia kubwa ni malumbano, muda wa kuzungumzia maendeleo umemezwa na siasa," alisema.

Aliongeza kwamba viongozi wameshindwa kuzungumzia namna ya kumaliza tatizo la chakula, fedha kushuka kila siku, umeme, mafuta na maendeleo ya wananchi na kutoa ushauri kwamba umefika wakati wa kukaa na kujiuliza kama wanachokifanya kitaliweka taifa salama ulikinganisha na ilivyokuwa kwa miaka 50 iliyopita.

Jaji Warioba alisema kutokana na hali Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa inapaswa kutambua kwamba demokrasia inayotumika iwe ya kujenga nchi sio kuligawa taifa au watu na kuwataka wanasiasa kushindanisha sera zao kwa wananchi na kuwaacha kufanya uamuzi kwa uhuru.

"Nchi hii sasa imekuwa ya kumaliza chaguzi na kuanza kampeni za uchaguzi mwingine, na sio hiyo tu, chaguzi ndogondogo haziishi mpaka leo limekuwa tatizo sugu linalowasumbua viongozi na kushindwa kufikiria namna ya kumaliza maadui watatu, hali hii ikiendelea hivi italeta uhasama na kuondoa umoja uliopo.

"Maendeleo yaliyopatikana kwa miaka 50 hii hatuwezi kuyakana, kwanza haikuwa kazi rahisi kupata uhuru, binafsi naitazama kila awamu ya urais naona Hayati Nyerere alikuwa na matatizo makubwa sana kama njaa ya mwaka 1984 lakini hawakukata tamaa, tulitumia umoja wa nchi kuyamaliza, leo hii hata viongozi wenyewe hawaelewani ofisini," alisema.

Alitoa ushauri kwa viongozi wa serikali ya sasa kwamba wanapaswa kuiga waasisi waliopigania uhuru kwa kudhubutu na kuondoa tofauti na mitazamo yao na kuungana na vyama, taasisi, mashirika kushambulia changamoto zilizopo ili kuepusha taifa na hali ya sitofahamu.

Kauli ya Msekwa

Naye Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi-Bara, Bw. Pius Msekwa alisema kuwa uwajibikaji wa viongozi waliopewa dhamana umepungua, licha ya kupewa zana zote za kazi tofauti na ilivyokuwa zamani.

Alisema hakuna sababu yoyote inayowafanya watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu kushindwa kuwasaidia wakuu wa nchi na kuwataka kuacha visingizio kama wanasiasa.


Tendwa anena

Naye Msajili wa Vyama vya Siasa, Bw. John Tendwa alisema tangu mfumo wa vyama vingi uanzishwe miaka 19 iliyopita, demokrasia imekua na imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuendesha nchi bila kuhatarisha amani ya nchi.

Bw. Tendwa alisema kuwa mchakato wa kuandaa katiba mpya unaendelea vizuri na utafanya mabadiliko katika sheria za kisiasa ili kutumika bila kuathiri usalama, amani na utulivu uliopo sasa.

Buriani awananga viongozi

Waziri Mstaafu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Bi. Batrida Burian alisema kuwa viongozi wa zamani na sasa ni tofauti, kwani wale wa zamani walikuwa na ushirikiano, ubunifu, bidii, uadilifu na uvumilivu na walifanya kazi bila kuhusisha siasa.

Bi. Buriani alisema kuwa asilimia kuwa ya viongozi wa sasa hawaleti taswira nzuri kwa wananchi na hivyo kuishauri serikali kufanya mabadiliko kuanzia getini na wafanya usafi kwa kuwa wamekuwa wakitoa kauli chafu wa wananchi wanaofika kupata huduma.

Alisema serikali inatakiwa kuwa na walinzi wake wenye maadili na sio kuchukua kwenye makampuni binafsi ya ulinzi ambayo hata chimbuko lao halijulikani.

Msiamo wa Anna Abdalla

Alisema maadili ya viongozi yameshuka kutokana na kutochukuliwa hatua za kinidhamu na kuitaka serikali kufanya maamuzi pale inapohitajika.

No comments:

Post a Comment