10 October 2011

Wajawazito wajifungulia kwenye ubao

Na Sammy Kisika, Sumbawanga.

WAJAWAZITO wa Kijiji cha Kilando Tarafa ya Kipeta wilayani Sumbawanga wameuomba uongozi wa halmashauri ya wilaya hiyo kunusuru masiha yao na watoto kutokana na
 miundombinu ya zahanati ya kijiji
hicho kuwa si rafiki kwa wajawazito.

Hali hiyo inayosababisha wajifungulie sakafuni.Wanawake hao waliokutwa juzi na gazeti hili wakiwa wameketi sakafuni wakisubiri huduma kutoka kwa mganga  wa zahanati hiyo, walisema wana hofu ya kupoteza maisha.

Mganga wa zahanati hiyo Bw. Dikson Kasapa, alisema anafanya kazi kwa kudra za Mwenyezi Mungu, kwani miundombinu ya zahanati hiyo si rafiki kwa utoaji wa huduma bora kwa wagonjwa.Bw. Kasapa alisema analazimika kuweka ubao  chini ya sakafu ambao wajawazito wanajifungulia, kwani hospitali haina kitanda wala godoro.

“Hapa hali si nzuri kwani hata mimi mwenyewe natoa huduma muda wote nikiwa nimesimama, hakuna kiti wala meza, kuna meza moja tu ndogo ambayo ndio nawekea maboksi ya dawa lakini pia hata wagonjwa wanaofika hapa wanalazimika kuketi sakafuni kutokana na kukosekana kwa viti au mabenchi ya kukalia” alisema Bw. Kasapa.

Alisema hata yeye yuko mbioni kuondoka, kwani hawezi kufanya kazi kwenye kituo hicho kulingana na mazingira yaliyopo.

“Angalia mimi na familia yangu ya watoto wawili tunaishi kwenye hiki chumba cha zahanati , hapa si mahali salama kwa kuishi kwani wagonjwa wanatibiwa hapa na mimi nalala hapo, upo uwezekano wa familia yangu kuambukizwa magonjwa, hii ni sehemu ya kutolea tiba na si ya kuishi” alisema.Alipoulizwa kuhusu hali ya zahanati hiyo  Mbunge wa jimbo la Kwela, Bw.Ignas Malocha, alikiri zahanati hiyo kuwa na hali ngumu.

“Vitu vingine tunaweza kukubali lawama, kwani huu ni uzembe wa wazi kwani suala nyumba ya kuishi mganga wa zahanati ni la wananchi wa eneo husika ambao wanatakiwa kujenga na serikali inakuja kumalizia kupaua, lakini hawa wamekaa tu, na hata kuchonga kiti cha mganga wao wanashindwa,” alisema Bw.Malocha

No comments:

Post a Comment