Na Eckland Mwaffisi, aliyekuwa Zanzibar
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Zanzibar, Bw. Vuai Ali Vuaia, amesema waasisi wa Muungano wa Tanzania Hayati Mwalimu Julius Nyerere na
Abeid Aman Karume, wanapaswa kuenziwa kwa vitendo ili kuharakisha maendeleo ya kijamii, kisiasa na uchumi.
Bw. Vuai aliyasema hayo juzi baada ya kupokea ugeni wa mabalozi zaidi ya 30 wanaoziwakilisha nchi zao nchini Tanzania ambao walitembelea Zanzibar ili kutoa heshima katika kabuli la Mzee Karume, lililopo Kisiwandui.
Alisema waasisi hao wanastahili heshima ya pekee kutokana na jitihada zao za kusimamia haki na kuimarisha misingi ya utawala bora ambao nguzo ya maendeleo katika Taifa lolote duniani.
Kiongozi wa Mabalozi nchini, Balozi Juma Mpango, alisema dunia inatambua mchango wa waasisi hao katika kupigania uhuru na kuunganisha Muungano ambao umepata mafanikio makubwa.
“Dunia imeamua kushiriki ziara hii ili kutoa heshima katika makabuli ya waasisi hawa, kimsingi tunatambua na kuheshimu mchango mkubwa waliotoa enzi ya uhai wao na tutaendelea kuwakumbuka daiwa,” alisema Balozi Mpango.
Alisema huwezi kuadhimisha miaka 50 ya Tanganyika bila kuwataja waasisi hao ambao walishirikiana katika mambo mengi ya msingi ambayo leo hii, matunda yake yameanza kuonekana kwa Watanzania wote.
Balozi Ali Karume alisema, amani, umoja na utulivu uliopo Zanzibar ni matunda ya Mzee Karume kutokana na jitihada zake za kuimarisha mizingi ya utawala bora.
Alisema Wazanzibar wanajivunia mambo mengi ambayo yametokana na busara za Mzee Karume ambaye aliwapenda wananchi na kuwawekea msingi mzuri wa maisha.
Kwa upande wake, Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, alisema ziara ya mabalozi hao ni kielelezo kuwa dunia inatambua mchango wa waasisi hao katika kuimarisha umoja na mshikamano wa nchi zao.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Bw. Bernard Membe, alisema Wizara yake imeamua kuadhimisha miaka 50 ya uhuru kwa kuandaa ziara ya mabalozi ambao pamoja na kutembelea makabuli ya waasisi wa Muungano, pia walitembelea vivutio mbalimbali vya utalii na makumbusho ya Mwalimu Nyerere, iliyopo Butiama mkoani Mara.
Vivutio hivyo ni Hifadhi ya Wanyama Serengeti iliyopo mkoani Mara, Oldpai George na Hifadhi ya Ngorongoro iliyopo mkoani Arusha.
No comments:
Post a Comment