19 July 2011

Walimu kutangaza mgogoro na serikali mwezi huu ikiwa...

Na Mwandishi Wetu

CHAMA cha Walimu Tanzania (CWT), kimeahidi kutangaza mgogoro mkubwa na serikali kama haitaeleza namna ya kulipa sh. bilioni 29.2 za madai mbalimbali ya walimu ndani ya
simu 12 zijazo.

Msimamo huo ulitolewa Dar es Salaam jana na Kaimu Katibu Mkuu wa CWT, Bw. Ezekiah Oluoch, wakati akizungumzia na waandishi wa habari.

Alisema ifikapo Julai 30 mwaka huu, kama Serikali itashindwa kueleza namna ya kulipa deni hilo, hakutakuwa na njia nyingine zaidi ya kutangaza mgogoro.

“Tunataka Serikali iseme zilipo pesa za walimu, waseme ziko katika fungu gani maana kila mwaka tunadanganywa lakini safari hii tunatangaza mgogoro na tunaomba CWT isilaumiwe katika hili,” alisema Bw. Oluoch.

Alisema katika bajeti ya mwaka 2010, Serikali ilidai kutenga sh. bilioni 22 za malipo ya walimu lakini fedha hizo haijulikani zilikwenda wapi.

“Nawaomba wabunge wanapojadili hotuba ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi wasaidie walimu kwa kuhoji zilipo fedha hizi ambazo tunazidai,” alisema.


Bw. Oluoch aliongeza kuwa, mapema Julai mwaka huu walimwandikia barua Katibu Mkuu Kiongozi, Bw. Philemon Luhanjo na kumpa siku 30 ili ateue kamati ambayo itakutna na CWT kujadili namna ya kulipa madeni ya walimu na kuepusha mgogoro unaokuja.

Alisema ingawa barua hiyo ilipokelewa Ikulu, hadi leo hakuna majibu yoyote yaliyotolewa na Bw. Luhanjo ambapo CWT imefanya jitihada mbalimbali pamoja na kukutana na chombo kinachojadili masuala ya walimu lakini hakuna matunda yaliyopatikana.

“Kwa mujibu wa sheria ya majadiliano ya pamoja katika utumishi wa umma ya mwaka 2003 na sheria ya ajira na mahusiano kazini ya mwaka 2004, inasema iwapo mwajiri atashindwa kulipa madeni ya mtumishi vyama vya wafanyakazi vinatakiwa kuitisha mgomo

“Nawaomba wanachama wa CWT wawe wavumilivu wakati huu tunapokabiliana na changamoto ya kudai madeni, tushikamane na tuwe kitu kimoja ili kudai haki zetu,” alisisitiza Bw. Oluoch.

Alisema Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi, Bi. Hawa Ghasia, Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda, waliahidi kwa nyakati tofautri kulipa madeni ya walimu lakini bado hayajalipwa.

Aliongeza kuwa, CWT imefanya jitihada za kuonana na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dkt. Shukuru Kawambwa lakini mkutano huo pia haukuzaa matunda.

Alisema inashangaza kuona Tume ya Usuluhishi iliagiza serikali ilipe madeni yote ya walimu hadi ifikapo Septemba mwaka 2010  lakini agizo hilo limepuuzwa.

Alisema Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI, Bw. George Mkuchoka, aliwahi kusema bungeni kuwa madeni ya walimu yatakuwa yamelipwa kabla ya Juni mwaka huu lakini hilo halijafanyika.

2 comments:

  1. Bwana Oluoch acha longolongo,huwa tunawaunga mkono hadi dakika za mwisho hatimaye MNATUSALITI.Kilichobaki ni walimu kufanya mgomo baridi kwa muda wa karne mbili hadi kieleweke.

    ReplyDelete
  2. Chama cha walimu si kitu si chochote.Wao nao waendelee tu kula michango ya walimu inayotolewa kila mwezi.Wangekuwa na dhamira ya dhati ya kuwatetea walimu wangepigania kodi ipungue kwa asilimia nzuri tu badala ya kung'ang'ania madeni yanayokwisha kwa muda mfupi na mwalimu kubaki hohehahe

    ReplyDelete