19 July 2011

Wafanyakazi wizara ya habari wapigwa msasa

Na Ismail Ngayonga, Maelezo

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Sethi Kamuhanda amewataka wafanyakazi wa wizara hiyo kufanya kazi kwa bidii na maarifa ili kutekeleza
vyema mipango na mikakati ya serikali.

Aliyasema hayo (jana), wakati wa mkutano wake na Wafanyakazi, Wakuu wa Idara,
Vitengo na Taasisi zilizopo chini ya wizara hiyo uliofanyika  Uwanja wa Taifa
jijini Dar es Salaam.

Bw. Kamuhanda aliongeza kuwa ili kufanikisha utekelezaji wa mikakati hiyo, ni wajibu
wa watumishi kushirikiana kwa pamoja na menejimenti ya wizara ili kuhakikisha
mapungufu yaliyopo yanapatiwa ufumbuzi.

Kwa mujibu wa Bw.  Kamuhanda alisema Ofisi yake imejipanga kukabiliana na changamoto
mbalimbali zinazojitokeza kwa watumishi ikiwemo uchakavu na ukosefu wa vitendea kazi
katika baadhi ya ofisi.

Bw. Kamuhanda alisema katika kipindi cha mwaka wa fedha 2010/11, watumishi hao wamefanya kazi nzuri na wakati mwingine katika mazingira magumu, lakini pamoja na mafanikio hayo watumishi hao hawana budi kuongeza kasi ya utendaji kazi.

Akifafanua zaidi Kamuhanda alisema bajeti ya mwaka wa fedha uliopita haikuwa nzuri
kwa wizara hiyo na serikali kwa ujumla, kwani fedha zilizotengwa kwa ajili ya
matumizi mengineyo zilipatikana kwa tabu na hivyo kupelekea baadhi ya miradi ya
maendeleo iliyopangwa kufanywa na wizara kutekelezeka kwa kasi ndogo.

“Tunafanya kazi vizuri, lakini malengo yetu ni kufanya vizuri zaidi ili kuzidi kile
tulichokifanya jana,”  alisisitiza, Bw. Kamuhanda huku akiwataka watumishi kubadilika
katika utendaji kazi.

Aliongeza kuwa wizara hiyo mwanzoni mwa   Agosti, 2011 inatarajia kuhamia katika
Ofisi mpya katika Jengo la PSPF eneo la Posta, ambapo Idara za Wizara hiyo
zinatarajia kuwepo katika sehemu moja tofauti na ilivyo sasa.

Alisema wizara hiyo inatarajia
kuongeza tija na morali ya utendaji kazi kwa watumishi wa wizara hiyo.

Alisema katika hatua nyingine, Bw. Kamuhanda alikemea tabia ya baadhi ya watumishi kubeba
mafaili yao binafsi yanayotunzwa katika ofisi za masijala, kwani kitendo hicho ni
kinyume cha kanuni, sheria na taratibu za utumishi wa umma.

“Utakuta madereva wanatumwa kuchukua mafaili na wakati mwingine hata mtumishi kubeba
faili lake na kulipeleka katika ofisi ya mkuu wake wa kazi, jambo hilo ni kosa
kisheria,” alisema, Bw. Kamuhunda.

Bw. Kamuhanda alisema ofisi ya masijala ndio injini ya kila ofisi ya serikali kwani
taarifa na kumbukumbu muhimu za watumishi wote huhifadhiwa eneo hilo, hivyo
hakutakiwi kwa mtumishi asiyehusika na masijala kuingia ndani ya ofisi hiyo.

Kwa upande wake Ofisa Vijana Mwandamizi kutoka Idara ya Vijana,Bw. Julius Tweneshe
alisema Idara ya Habari haina budi kutumika kikamilifu kutangaza mafanikio ya
kisekta yaliyofikiwa na kila idara na taasisi iliyopo chini ya Wizara ya Habari,
Vijana, Utamaduni na Michezo.

“Katika maonesho ya wiki ya utumishi yaliyomalizika hivi karibuni, banda la Idara
ya Habari la nchini Kenya lilivutia watazamaji wengi, na tukiangalia mifano iliyopo katika nchi nyingine tutaiona nchi ya Kongo leo hii imeweza kujitangaza vyema
kupitia muziki wake na hii ni changamoto kwetu pia” alisema, Bw.  Tweneshe.

Alitoa changamoto kwa menejimenti ya wizara kuwapandisha vyeo watumishi wake
kwa wakati badala ya mtumishi kukaa na cheo kimoja kwa kipindi kirefu. 

No comments:

Post a Comment