14 July 2011

Wadau wa ngumi watakiwa kudhamini michuano

Na Mwali Ibrahim

UONGOZI wa ngumi za ridhaa mkoa wa kimichezo wa Ilala, umewataka wadau mbalimbali kujitokeza kuwadhamini katika mashindano ya kuhamasisha ngumi hizo kwa
mkoa huo.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Kocha Mkuu wa mkoa huo, Habibu Kinyogoli alisema wanahitaji wadau mbalimbali kujitokeza kuwasaidia mahitaji mbalimbali ikiwemo zawadi kwa ajili ya washindi pamoja na maji.

"Licha ya zawadi na maji, pia tunawaomba wadau wajitokeze kuangalia mapambano hayo ili kuwatia moyo na kuwapa hamasa wachezaji kushiriki katika kuhamasisha ngumi hizo," alisema Kinyogoli.

Alisema wamekuwa wakiendesha mashindano bila kutoa zawadi na hata kuwepo na maji ya kutosha kwa wachezaji, ambao wanashiriki huku wakiwa hawapo katika hali nzuri ya mashindano.

Kinyogoli alisema, wameandaa mashindano mengine ya kuhamasisha mchezo huo ambayo yanatarajia kufanyika Jumapili katika Ukumbi wa Panandi panandi uliopo Ilala, Dar es Salaam.

Alisema katika mashindano hayo jumla ya mabondia 60, watachuana wakitokea katika klabu tano za ngumi, ambazo ni Ashanti, Matimbwa, Bigright, Midizini na Amana.

Kocha huyo alisema katika kuonesha njia mdau wa ngumi, Halima Kaubanika ametoa msaada wa katoni kumi za maji ya kunywa kwa ajili ya kutumika siku hiyo.

No comments:

Post a Comment