14 July 2011

Rostam ajivua gamba

Na Waandishi Wetu, Igunga na Dar
Bw Rostam Aziz
MBUNGE wa Igunga, Bw. Rostam Aziz amekuwa mwanachama wa kwanza wa Chama cha Mapunduzi (CCM) kujivua gamba baada kuachia ngazi nyadhifa zake zote alizonazo kupitia
chama hicho ikiwemo kiti cha Ubunge.

Uamuzi huo umekuja wakati siku 90 zilizotolewa na chama hicho kikiwataka watuhumiwa wa ufisadi wajivue gamba la sivyo wangefukuzwa zikiwa zimetimia, hivyo kusubiri uamuzi wa Halmashauri Kuu ya CCM itakayokutaka hivi karibuni.

Hata hivyo, mapema akizungumza na wazee wa Jimbo la Igunga jana, Bw. Aziz alisema amefikia uamuzi huo wa kuachia nafasi zote za uongozi alizopata kwa tiketi ya CCM na uamuzi huo haukutokani wala kumaanisha kukubaliana na shinikizo la utekelezaji wa dhana ya kujivua gamba.

Alisema hiyo ni dhamira ya dhati ya kuachana na 'siasa uchwara' ili atumie muda wake kushughulika na biashara zake, kwani tangu matukio yanayogusa jina lake yaanze kutokea miezi michache tu baada ya Serikali ya Awamu ya Nne inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete kuingia madarakani kwa mara ya kwanza mwaka 2005 imekuwa ikimwathiri kibiashara.

Alisema baada ya kukaa na wanafamilia yake, marafiki na washirika wake wa kibiashara ameona halitakuwa jambo la busara kuendelea kuvutana na viongozi wa chama chake na wanachama wenzake wa CCM katika mambo ambayo yanaweza kumalizwa kwa njia muafaka.

"Sina budi niwaeleze kwamba, mbali ya athari za kisiasa na kifamilia, vita vya ovyo vya kisiasa kama hivi tunavyoviendesha na kuviendeleza ndani ya CCM na ndani ya nchi yetu huwa vina athari kubwa katika ulimwengu wa kibiashara," alisema Bw. Aziz.

Alisema kama ilivyo katika maeneo mbalimbali nchini, mafanikio makubwa tuliyoyapatikana katika nyanja za elimu, afya, makazi bora na kilimo katika kipindi chote akiwa mbunge wa Igunga kwa miaka 18 wananchi wake wamekuwa na imani kubwa na kuunga mkono kwa dhati naye alijitahidi kwa kadiri alivyoweza kutimiza matarajio ya wananchi wa jimbo hilo.

Alisema miongoni mwa mafanikio makubwa waliyoyafikia kupitia ushirikiano wake na uongozi wa pamoja ni kwamba, mwaka 1994 Igunga ilikuwa ni wilaya ya mwisho kwa maendeleo mkoani Tabora lakini leo ndiyo ya kwanza, ina taa za barabarani, bima ya afya kwa kila kaya, zahanati kila kijiji na shule nyingi kuliko idadi ya kata zilizomo kwenye wilaya.

Alisema katika kipindi chote cha utumishi wake wazee hao walikuwa mhimili muhimu ambao umemwezesha kutimiza wajibu kwa bidii kubwa, maarifa na nidhamu ya hali ya juu akitambua namna ambavyo wamekuwa na imani kubwa juu yake.

Alisema wananchi wa Igunga wamekuwa wakifuatilia kwa karibu hali ya siasa nchini na matukio mengine ndani ya CCM ambako yeye alikuwa mwanachama na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) akiwakilisha Mkoa wa Tabora.

"Nafanya hivyo nikitambua vyema kwamba, kama si nyinyi wazee wangu na wengine wengi ambao hatuko nao hapa leo kwa sababu mbalimbali, ambao mmekuwa na imani kubwa nami nisingeweza kufikia hapa nilipofika sasa," alisema.

Anatambua na kuheshimu ukweli kwamba katika kipindi chote cha ubunge wake wananchi wa Igunga wamekuwa na imani kubwa na kumuunga mkono kwa dhati, anaamini kwamba kwa upande wake pia amejitahidi kwa kadiri alivyoweza, kutimiza matarajio ya wananchi wa Igunga.

"Naamini kwamba katika kufuatilia kwenu mtakuwa mmebaini kuwapo kwa matukio ambayo kwa namna moja au nyingine yamekuwa yakitokea huku yakiligusa jina langu na wakati fulani nafasi yangu kama kiongozi wa CCM," alisema.

Alisema alipokuwa katika ziara zake jimboni na wakati mwingine wananchi walipowasiliana naye kwa njia mbalimbali wamekuwa wakionesha kuguswa, kushtushwa na kutaka kujua kulikoni kuhusu mambo hayo yanayotokea naye siku zote amekuwa mwepesi kuwaeleza kuhusu kila kinachotokea ili kuwaondoa hofu.

Bw. Aziz alisema pia kuwa amekuwa akiwahakikishia kwamba masuala yasiyo na msingi hususani yale yanayogusa siasa za kitaifa hayawezi kuondoa katika mstari sahihi wa kuwahudumia wananchi wa Igunga, wakiwamo wazee hao ambao walimwamini na kumtuma kuwawakilisha.

Alisema anaamini na ataendelea kuamini kwamba walifanya uamuzi sahihi wa kuyapuuza matukio hayo kwani mbali ya kuendelea kutimiza malengo mbalimbali yaliyokuwamo katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM, pia wananchi hao waliendelea kumwamini kwa nafasi yake ya kuwa mwakilishi wao bungeni na hata wamruhusu kubeba jukumu jingine kubwa la kuwa Mjumbe wa NEC aliyewakilisha mkoa wa kihistoria wa Tabora.

'Wazee wangu, nyinyi ndiyo watu mnaolifahamu vyema jimbo letu la Igunga na hakika nyinyi ni sehemu muhimu ya watu wanaojua historia ya kisiasa ya Mkoa wa Tabora kwa miaka mingi hata kabla ya kuja kwa mfumo wa vyama vingi hapa nchini," alisema Bw. Aziz.

Alisema alifanya kazi ya kuijenga CCM katika mazingira yenye mizizi hasa ya upinzani akiwa mbunge na mjumbe wa NEC kutoka Mkoa wa Tabora haijapata kuwa rahisi na itaendelea kuwa ngumu na ambayo mapambano yake ni makali.

Matunda ya kazi hiyo kubwa yanaonekana pamoja na kuwa kitovu cha kihistoria cha siasa za upinzani, Tabora ndiyo mkoa pekee katika eneo hili ambao unaongozwa na wabunge wote kutoka CCM baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana na hata kabla ya hapo.

Alisema ukiacha mafanikio makubwa yaliyopata katika jimbo na wilaya ya Igunga, kuna mambo mengine ya msingi ya kujivunia hivyo kwa moyo wa dhati na unyenyekevu mkubwa anawapongeza kwa namna walivyojitoa kukipigania na kuitetea CCM kwa ari na nguvu ya kipekee.

Alisema anakubaliana na uongozi wa Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete ya kuamua kwa kauli na nia moja kujitathmini na kufanya mabadiliko makubwa ya kimfumo yenye lengo la kukiwezesha chama kiendelee kuwa pekee kinachoaminiwa na kuungwa mkono na Watanzania wengi.

Dhamira ya mwelekeo huo wa kufanya mabadiliko ya ndani ya CCM yaliyotangazwa na Mwenyekiti Rais Kikwete wakati wa kilele cha maadhimisho ya miaka 34 ya kuzaliwa kwa CCM, mjini Dodoma hotuba yake  aliyafananisha mabadiliko hayo na tabia ya kawaida na ya asili ya nyoka na wanyama wengine kadhaa ya Kujivua Gamba anaungana nayo.

Alisema hatua ya kwanza ya utekelezaji wa azimio hilo na mwelekeo huo sahihi ilifanyika mjini Dodoma wakati wa kikao cha Kamati Kuu ya Taifa ya CCM ambacho yeye alikuwa mjumbe.

Wakati wa kikao hicho, wajumbe wote wa Kamati Kuu na wale wa Sekretarieti ya CCM ya wakati huo kwa kauli moja walikubaliana kujiuzulu, lengo likiwa ni kumpa mwenyekiti fursa nzuri ya kufanya mabadiliko ya uongozi yatakayotoa nafasi ya kupata mwelekeo mpya wa chama.

"Wazee wangu, tulifanya hivyo tukionesha kuunga mkono kwa asilimia 100 kile ambacho bado naendelea kuamini kuwa ni mawazo sahihi na yenye mwelekeo thabiti ya Mwenyekiti wetu ambayo kwa kiwango kikubwa yalikuwa yakiakisi matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa urais, ubunge na udiwani wa Oktoba mwaka jana," alisema Aziz.

Alisema ingawa ni kweli Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana umekirudisha CCM madarakani kwa kukipa ushindi mkubwa katika uchaguzi wa urais, ubunge na udiwani kwa Tanzania Bara na Zanzibar, kiwango cha ushindi CCM ilichopata kimeonesha waziwazi dalili za wananchi kupunguza imani yao kwao kulinganisha na ilivyokuwa mwaka 2005.

"Tungekuwa ni chama cha siasa cha ovyo iwapo tungepuuza kupungua kwa kura za rais kutoka zaidi ya asilimia 80 tulizopata mwaka 2005 hadi kufikia asilimia 61 mwaka jana kiwango ambacho ni pungufu kwa asilimia 20 ya kura katika kipindi cha miaka mitano tu, hasa ikizingatia ukweli kwamba mgombea urais ni mtu yule yule," alisisitiza Bw. Aziz.

Alisema kingekuwa chama cha siasa kilichokosa umakini iwapo wangekaa pasipo kuchukua hatua zozote za kujiimarisha baada ya matokeo ya Uchaguzi Mkuu kuonesha wazi kukua kwa upinzani ambao umeongeza idadi ya wabunge na madiwani katika pande zote mbili za muungano.

Alisema kwa sababu ya kutambua ukweli kwamba hakuna haki isiyo na wajibu, yeye na wenzake waliokuwa katika Kamati Kuu waliona ulazima, haja na umuhimu wa kukubali kwa kauli moja wito wa kuwataka tujiuzulu ikiwa ni hatua moja ya kujipanga na kukijenga upya chama hicho.

Alisema kilichotokea baada ya kujiuzulu kwao kila aliye ndani na nje ya CCM amekisikia na anakifahamu, chama kilipata safu mpya ya uongozi iliyotokana na kuundwa kwa Sekretarieti inayoongozwa na Katibu Mkuu mpya, Bw. Wilson Mukama na Kamati Kuu iliyokuwa na sura tofauti na ile ya awali.

Wakati tukitafakari na kuangalia mustakabali mpya wa kisiasa ndani ya CCM, alisema ghafla yalianza kutokea mambo ambayo chokochoko zake zilianza kusikika tangu wakiwa ndani ya Kamati Kuu ambayo ilijiuzulu baadaye.

Mara tu baada ya kumalizika kwa kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ambacho kilichagua wajumbe wapya wa Kamati Kuu na kuidhinisha uundwaji wa Sekretarieti mpya, dhana ya kujivua gamba ambayo naamini Mwenyekiti Kikwete aliianzisha kwa nia njema ilianza kuenezwa ikichukua tafsiri na mwelekeo tofauti na ule wa awali.

Alisema wajumbe wawili wa Sekretarieti, Naibu Katibu Mkuu (Tanzania Bara), Bw. John Chiligati na Katibu wa Idara ya Itikadi na Uenezi, Bw. Nape Nnauye, walisikika wakitangaza kwamba Halmashauri Kuu ya Taifa ilikuwa imefikia uamuzi wa kuwapa siku tisini wale walioitwa watuhumiwa wanaokabiliwa na tuhuma za ufisadi ndani ya chama kujitoa katika nafasi zao za uongozi vinginevyo watafukuzwa na chama.

Baada ya awali kuwaeleza waandishi wa habari kwamba majina ya watuhumiwa hao yalikuwa yakifahamika kutokana na kuhusishwa katika kashfa tofauti kama zile za Richmond, EPA na ununuzi wa rada, mwishoni viongozi hao walikaririwa wakiyataja majina ya wanasiasa watatu kuwa ndiyo ambao walikuwa wakilengwa na maamuzi hayo, likiwamo la Mbunge wa Igunga.

"Mshangao na mshituko wangu haukusababishwa na kutajwa kwa jina langu, la hasha, bali namna uamuzi halisi wa NEC na hususani dhana nzima ya kujivua gamba ilivyoweza kupindishwa na wajanja wachache na kisha kuendeshwa kwa maslahi binafsi ya kikundi fulani cha watu," alisema Bw. Aziz.

Kauli yake

Wazee wangu, nimetafakari sana na kimsingi nimefikia hatua ya kupima yale ambayo yamekuwa yakisemwa na kuandikwa juu yangu na ambayo kwa mtazamo wangu unaoungwa mkono na wanafamilia yangu, marafiki zangu na washirika wangu wa kibiashara walio ndani na nje ya nchi, naona umefika wakati muafaka wa kuchukua hatua.

Kwa sababu ya kutambua uzito wa hatua ninazokusudia kuzichukua, niliona halitakuwa jambo la hekima hata kidogo iwapo ningefanya hivyo pahala pengine popote bali hapa Igunga mbele ya nyie wazee wangu.

Baada ya kukaa na wanafamilia yangu, marafiki na washirika wangu wa kibiashara niliona halitakuwa jambo la busara hata kidogo kuendelea kuvutana na viongozi wa chama changu na wanachama wenzangu wa CCM katika mambo ambayo yanaweza kumalizwa kwa njia muafaka.

Wazee wangu, sina budi niwaeleze kwamba, mbali ya athari za kisiasa na kifamilia, vita vya ovyo vya kisiasa kama hivi tunavyoviendesha na kuviendeleza ndani ya CCM na ndani ya nchi yetu huwa vina athari kubwa katika ulimwengu wa kibiashara.

Kutokana na ukweli huo na sababu zote hizo basi, kwa moyo wa dhati na kwa nia thabiti, hatua ya kwanza niliyoiona kuwa ninapaswa kuichukua ilikuwa ni hii ya kuitikia wito unaotokana na msukumo wa ndani ya nafsi yangu wa kuamua kukomesha kabisa malumbano na mivutano isiyo na manufaa kwangu binafsi, kwa viongozi wa chama changu na chama chenyewe.

Msukumo huo si mwingine bali ni ule wa kuamua kuachia nafasi zangu zote za uongozi ndani ya chama, nikianzia na ile ya ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa nikiuwakilisha Mkoa wa Tabora na hii ya ubunge wa Igunga ambazo kama si kwa baraka za chama changu nisingelikuwa nazo.

Napenda kuliweka hili sawa sawa. Uamuzi wangu wa kuachia nafasi zangu zote za uongozi nilizopata kwa tiketi ya CCM haukutokana na wala haumaanishi kukubaliana na shinikizo lililopotoshwa kuhusu azma ya utekelezaji wa dhana ya kujivua gamba, la hasha, bali dhamira ya dhati ya kuachana na siasa hizi uchwara (gutter politics) na kutumia muda wangu kushughulika na biashara zangu.

Waandamana mitaani, wazirai

Mara baada ya kutoa tamko hilo hilo, vurugu ziliibuka mjini hapa baada ya vijana wenye mabango kujitokeza wakidai wanapinga kujiuzulu kwake, wakitaka kumshinikiza aendelee na nyadhifa zake kwa kuwa bado walikuwa wanampenda.

Wengine walizirai  na kupelekwa hospitali, akiwamo katibu Mwenezi wa kata ya Chabutwa, Bw. Athuman Mihayo, Mwenyekiti wa UV-CCM Nzega, Bw. Daud Ng'onge na wanachama wawili, Zainab Athumani na Catherine Mabula.

Katika purukushani hiyo, mkazi mmoja wa Igunga aliyepiga simu chumba cha habari Majira na kujitambulisha kama Mahame Ahmed alidai kukamatwa na polisi na kunyang'anywa bango lake lilieleza hisia tofauti za wenzake.

"Mimi nilikuwa na mawazo tofauti, wengine waliletwa wakiwa na mabango ya kuonesha wanapinga uamuzi wake, mimi nikaonesha bango langu likiwa na ujumbe unaosema 'Tanzania bila Rostam inawezekana; na Igunga bila Rostam inawezekana'.

"Ninacholalamika, ni kwamba sikutendewa haki. Hao wengine wameruhusiwa kuonesha hisia zao, mimi nimechukuliwa, nikahojiwa na kuachiwa baadaye lakini bango langu wamelichukua polisi," alisema.

Maoni ya Wabunge

Mbunge wa Simanjiro, Bw. Christopher Ole Sendeka alimpongeza Bw. Aziz akisema kuwa ameonesha ujasiri na nidhamu kwa chama chake.

Naye Mbunge wa Singida Mashariki alisema kuachia ngazi wa Bw. Aziz ni ishara kuwa yale yaliyosemwa na chama chake, CHADEMA kilipota watuhumiwa 11 wa ufisadi yametimia, kwa mmoja wao kuachia ngazi, bado wenzake 10.

25 comments:

  1. siku zote mwizi hupendwa kwao. ndio maana LOWASSA, CHENGE pia wanapendwa kwao. mzee MALECELA hakuwa mwizi ndio maana kwao sio maarufu hadi leo. TUNAHITAJI VIONGOZI KAMA MALECELA kwa ajili ya taifa la leo. kupendwa kwa rostam ni kutokana na vijisenti vya wizi ambavyo hata hivyo havifanyi mambo sustainable....tunataka list of shame..wale 10 wa mwembeyanga wote wawajibike....

    KUJIUZULU NI KLA KWANZA. KUWAJIBIKA MBELE ZA SHERIA NI JAMBO LINGINE. ROSTAM SASA APELEKWE KIZIMBANI KUJIBU MASHTAKA YAKE.

    ReplyDelete
  2. Bado Chenge na Lowassa

    ReplyDelete
  3. Nyerere anapendwa kwao Tanzania naye ni Mwizi?
    Acheni maneno watu wenye akili wanafuatilia mambo yanayo tokea hapa ncnini.

    Rostam na wenye rangi wenzake wamekuwa target ya watanzani(wafanyabiashara) weusi kwamuda mrefu sasa.

    Nakutakia kila laheri rostam si wewe tu mko wengi mnao pigwa vita kwa sababu ya rangi yenu Mungu anajua na wenya Akili tunajua.

    ReplyDelete
  4. What goes around comes around,nani asiyejua jinsi jamatini zinavotumika kuchangisha peas kila ibada kwa ajili ya kuandaa viongozi wasio watanzania wahonge wananchi ili wawapende?Hata wakina Pabro escoba wanapendwa sana na jamii zao kwani utumia mapato ya biashara haramu ya madawa kupata regitimacy kwa jamii,ROstam sio mzalendo na hana uchungu na nchi hii,let him go, we need patriot Tnazanians in the parliament.

    ReplyDelete
  5. kewli c kila anaependwa kwao ni mwizi. ikiwa hivo bs dr slaa, mbowe, nao ni wezi coz dr slaa alipoamua kugombea urais na kuacha ubunge wananchi walilalama

    ReplyDelete
  6. Chenge na Lowassa igeni mfano wamwenzenu,kwani watanzania tumechoka kusikia migogoro kila kukicha,hatujengi nchi bali tuna umiza watanzania masikini.MTOKE.

    ReplyDelete
  7. CCM inapaswa kuwaajibisha hao walio baki kwa maslai ya Taifa letu muda wa kubembelezana umepitwa nawakati,nchi yetu bado ipo nyuma kimaendeleo.Yote nisababu yawatu wachache wasiyo kuwa na uchungu wamaisha ya Mtanzania.Jamani mnataka tufe ndo mjuwe watnzania tunahali ngumu?

    ReplyDelete
  8. Mr,Lipumba nakupa pole kwa kuumwa nakutakia kheri na nafuu upone haraka, uje tujipange jimbo hili ni letu liko wazi la Igunga maana ktk chaguzi iliyopita CDM hakuwemo kwa hiyo hana ubavu wa kulitwaa tujipange haraka tukafuwe wanachama toka CCM.CUF tulipata asilmia 23.1,ktk kinyan'ganyiro kilichopita.Kufa kufaana

    ReplyDelete
  9. Ningependa kuona waliosalia wanawajibishwa na chama kwani muda wa siku 90 walizopewa umeshakwisha.Chama kikifanya hivyo kitarudisha imani kwa kiasi fulani.

    ReplyDelete
  10. kujivua gamba kwa Rostam Azizi kuwa ni chachu kwa viongozi wa serikali kuachana na wizi wa mali za wananchi vinginevyo aibu na fadheha ni juu yao siku zote za maisha yao na kwa Mungu ni adhabi kuwa sana. viongozi wajifunze kwa Rostam na waachane na ufisadi maana haumpendezi Mungu wala Mwanadam

    ReplyDelete
  11. ROSTAM POLE SANA ULICHOPANDA NDICHO ULICHOVUNA, NA SHERIA ITACHUKUA MKONDO WAKE. usifikiri kujivua gamba umepona kutoka mkononi mwa mwindaji

    ReplyDelete
  12. Nakukubali sana Rostam nakupongeza pia kwa uamuzi mgumu ulio uchukua hao hii inaonesha nijinsi gani siasa ulivyo iwezea Big up Muheshimiwa Rostam AZIZ.

    ReplyDelete
  13. Zitto anapendwa kwao. je ni mwizi? Kafulila anapendwa kwao. je ni mwizi? Slaa anapendwa kwao. je ni mwizi?.Ole Sendeka anapendwa kwao je ni mwizi? mnyika anapendwa ubungo. je ni mwizi? Msilete mifano ya kwenye gazeti la mwananchi mkatuchafulia gazeti letu. mifano ya vijiweni pelekeni klatika gazeti la mwananchi. sio majira

    ReplyDelete
  14. Hiyo 'lead' inapotosha. Rostam ni gamba. Amekuwa gamba la kwanza kutoka. Gamba haliwezi kuvua gamba.

    ReplyDelete
  15. Uko sahii,Rostamu ndiye gamba,yeye ndiye kavuliwa toka Chama Cha Magamba.Pia Rostam ni msanii,nasikia alilipa watu pesa ili wamlilie,kama unabisha hayo mabango yaliyojitokeza ukumbini mara tu baada ya kumaliza hotuba yaliandaliwa saa ngapi? ina maana kulikuwa tayari na maandalizi ya tukio ilo,mibaba mizima inajiangusha chini inalia kama watoto!

    ReplyDelete
  16. Uko sahii,Rostamu ndiye gamba,yeye ndiye kavuliwa toka Chama Cha Magamba.Pia Rostam ni msanii,nasikia alilipa watu pesa ili wamlilie,kama unabisha hayo mabango yaliyojitokeza ukumbini mara tu baada ya kumaliza hotuba yaliandaliwa saa ngapi? ina maana kulikuwa tayari na maandalizi ya tukio ilo,mibaba mizima inajiangusha chini inalia kama watoto!

    ReplyDelete
  17. Yote yawezekana, ushabiki, utaahira wa maono na mitizamo. Si kweli wapendwa kwao wote ni wezi ila hili linakuja pale ambapo mtu anajua yeye ni mhalifu anatumia hadhi ya uhalifu kusafisha jina lake. Kwani wananchi wa Igunga hawajui kama Rostam ni fisad? mbona walipekuwa wanapewa hela wanapokea bila kuhoji? Ni wabunge wangapi wenye uwezo huo wa kugawa vijihela? Hao waliokuwa wanamlilia ni wanafiki tena sana, hawamtakii heri mwenzao ndo maana ukiwaangalia wote walijigalagaza wana vitambi vya rushwa walivyovipata kwa njia ya kifisadi. Hongera Rost Tamu Lazizi kwa uhamuzi uliochukua, umeshaifaid sana serikali ya CCM. Nenda baba nenda kapumzike mwalimu wa mafisad

    ReplyDelete
  18. Tena baba moja na kitambi kikubwa linalia kilo utadhani mtu kafa,uwiii,limenichefua kweli.Kilio cha kinafiki tu,wanalilia vijisenti alivyokuwa anawapatia na kujikomba kwao,sasa wanaona Rostamu hatakuwa anawapa ofa za pilau walizozoea.Kwani maendeleo ya Igunga kaleta yeye? si ni fedha za serikali.Wangejua ufisadi aliofanyia taifa ili wala wasingejifanya kumlilia.Lakini sawa hata wenye watoto vibaka ambao wakikwapua wanamletea mama,siku mtoto kibaka akichomwa moto mama ataomboleza sana na kudai mwanae wanamuonea bila kujiuliza vile vidani alivyokuwa analetewa na mwanae alikuwa anavitoa wapi?

    ReplyDelete
  19. izo zote mbwembwe tu!!!la maana tumshukuru tu kwa uamuzi wake wa kutuachia nchi yetu koz in 1 way or another ana sauti kuliko raisi wetu na tusi expect kesi yake itaenda popote..ona Chenge imeishia wapi?izi ni propaganda tu..Bwana Rostam tunakushukuru sana labda tutaanza kuhema tena..wheew!

    ReplyDelete
  20. Mwizi hawezi kuaxha alichoiba kama aliyeibiwa hajajua kaibiwa wapi? kujivua gamba kwake kunaashiria kutega sehemu nyingine ili azidi kutuumiza zaidi.
    Tunatakiwa kuwa macho zaidi ili tuone na waliobaki na wengine ambao hawajatajwa wanawajibika

    ReplyDelete
  21. Mhmmm!!!Mimi yangu macho kwa mwenye macho haambiwi tazama. Ili nchi inakwenda kubaya inaitajika umakini katika kufanya maamuzi kwani kujiuzuru kwake tunaweza fikiri tunajenga tukajikuta tunaingia kwenye matatizo makubwa katika nchi na chama pia BUSARA A HALI YA JUU ZINAITAJIKA KATIKA MAAMUZI

    ReplyDelete
  22. majira na nyakati za kujiuzuru yalishafika maana kila lenye mwanzo halikosi kuwa na mwisho ameshajishibia mapesa ya kumtosha mpk mwisho wake wa dunia hata tulikisema ni bure tuu hakuna wa kumfanya chocho maana yeye ndio alikuwa rais wa nchi hii kwani hamjui?

    ReplyDelete
  23. Nyie mnao mtaja taja Lowassa, mnataka afanye nini? kuna uamuzi mgumu kama kuuachia uwaziri mkuu? halafu ubatizo wa hiyo richmond sio symbion? Lowassa is a total man na kamwe hatajiuzulu. Wengi CCM wanatakiwa kujiuzulu na najua mnajua kuanzia level ipi.

    ReplyDelete
  24. Siku sio nyingi Rostam atahamishia biashara zake kwao Iran awaachie siasa zenu na siasa zenu za maji taka na nchi yenu inayovunwa kama shamba la bibi.

    ReplyDelete
  25. Huu ndiyo mwnzo wa mwisho wa CCM. Mungu ibariki Tangayika.

    ReplyDelete