21 July 2011

Redd's Miss Ilala 2011 wapima UKIMWI

Na Addolph Bruno

WAREMBO wanaowania taji la Red's Miss Ilala jana wamepima UKIMWI na kuwashauri Watanzania kuondokana na uwoga wa kupima ili waweze kupanga maisha yao
ya baadaye.

Washiriki hao waliionesha jamii mfano huo jana na wakawasifu waandaaji wa Miss Ilala kuanzisha tukio hilo zuri kwa jamii.

Wakizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, mara baada ya kupima afya zao katika ofisi za AMREF, warembo hao walisema ikiwa kila Mtanzania atajijua afya yake wataishi maisha ya furaha kama walivyofanya wao.

Mmoja wa warembo hao Alexia William, alisema ataitumia fursa hiyo kuwashawishi wengine kujua afya zao na kuwaomba Watanzania kuiga mfano wao.

"Kabla ya kufika hapa niliwahi kupima mara moja, lakini nilikuwa bado nina wasiwasi kwa sababu bado nilitakiwa kufanya hivi, ila sasa angalau nawaomba Watanzania wafanye hivi wasiogope, kwani wanapata fursa ya kuchagua namna ya kuishi na kupanga mambo yao," alisema.

Katika hatua nyingine, warembo hao wamekabidhiwa bendera ya taifa na Serikali ya Halmashauri ya Wilaya ya Ilala kuondoka Dar es Salaam leo kwenda mkoani Arusha na baadaye Nairobi, Kenya ambako watashiriki shughuli za kijamii.

Kiongozi wa kambi ya warembo hao, Regina Joseph alisema kesho watakuwa Arusha na keshokutwa watakuwa Nairobi kabla ya kurejea nchini Mei 23 mwaka huu kwenda mkoani Manyara, ambapo Julai 24, mwaka huu watarejea Dar es Salaam na siku hiyo  watashindana kusaka vipaji 'Miss Talent 2011' katika hoteli ya Savana Lounge.

Akizungumza mara baada ya kuwakabidhi bendera, Mkurugenzi wa manspaa hiyo Ogare Salimu, aliwapongeza wanyange hao na kuwataka kuwa mabalozi wa kweli kwa maendeleo ya wilaya ya hiyo.

No comments:

Post a Comment