21 July 2011

Mwanafunzi Magogoni kortini kwa kubaka

Na Rehema Maigala

MWANAFUNZI wa Chuo cha Utumishi wa Umma Magogoni, Rajabu Yusuph (19), amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni kujibu mashtaka ya
kumbaka binti mwenye umri wa miaka 16.

Mbele ya Hakimu Suzan Makabwa ilidaiwa na Mwendesha Mashtaka Inspekta wa Polisi Benedict Nyagabona kuwa Julai 16, mwaka huu, huko Magomeni Wilaya ya Kinondoni mshtakiwa alimbaka mtoto wa kike wa kumsababishia maumivu sehemu za siri.

Mshtakiwa alikana mashtaka hayo na yupo nje kwa dhamana mpaka kesi hiyo itakapotajwa tena Agosti 1, mwaka huu.

Pia, Babilon Alex (21), mkazi wa Kunduchi amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni kujibu mashtaka ya kuvunja na kuiba katika ofisi ya Inter Press Tanzania Limited.

Mbele ya Hakimu Hilda Lyatuu ilidaiwa na Mwendesha Mashtaka Inspekta wa Polisi Mohamed Kilongo kuwa, Julai 16 mwaka huu, huko Salasala Wilaya ya Kinondoni mshtakiwa alivunja ofisi hiyo na kuiba vitu mbalimbali ambavyo thamani yake ni sh.17,300,000.

Mshtakiwa alikana mashtaka hayo na kuachiwa kwa dhamana mpaka kesi hiyo itakapotajwa tena Agosti 2, mwaka huu.

Wakati huo huo, Gerald  Nathanael (22), mkazi wa Mbezi Msigani amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni kujibu mashtaka la kujeruhi.

Mbele ya Hakimu Kwey Rusemwa ilidaiwa na Mwendesha Mashitaka Inspekta wa Polisi Benedict Nyagabona kuwa, Mei 27, mwaka huu, mshtakiwa alimjeruhi mlalamikaji Leonard Bova kwa kumpiga na kipande cha chuma sehemu mbalimbali za mwili wake.

Mshtakiwa alikana mashtaka hayo na yupo nje kwa dhamana hadi Agosti 2, mwaka huu.

No comments:

Post a Comment